Na. Moses Mpunga, DODOMA
WATUMISHI wa Serikali mkoani Dodoma wamemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha maslahi ya watumishi wa Umma kwa kupandisha mishahara kwa asilimia 23.3 pamoja na posho mbalimbali.
Shukrani hizo zilitolewa na Mtunza Kumbukumbu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Imelda Matofali katika hafla fupi ya kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuboresha maslahi ya watumishi katika ukumbi wa mikutano wa PSSSF jijini hapa.
Matofali akizungumza kwa niaba ya watunza kumbukumbu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, alimshukuru Rais kwa kuwakumbuka watumishi wa kada za chini. Alisema kuwa Rais amewakumbuka kwa kuwaongezea mishahara pamoja na posho jambo ambalo halikuwahi kufanyika kwa muda mrefu. "Kama mnavyojua Rais wetu ni mama na sifa kubwa ya mama ni kuwakumbuka watoto wake. Hivyo, tunamshukuru sana mama kwa kutukumbuka na sisi tunamuahidi kuchapa kazi kwa nguvu zetu zote" alisema Matofali.
Akiwawakilisha Watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Afisa Mtendaji Kata ya Uhuru, Christina Mpete (pichani juu) alimuhakikishia Rais Samia Suluhu Hassan kuwa watumishi wataongeza juhudi katika kufanya kazi na kuwa atembee kifua mbele wao wapo nyuma yake na hawatamuangusha. Alisema kuwa ongezeko hilo la mishahara na posho limeongeza morali ndani ya watumishi wa Halmashauri hiyo.
"Mama yetu tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu akulinde na akupe afya njema ili uendelee kuchapa kazi na kutuhudumia watanzania" aliongeza Mpete.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Mkoa wa Dodoma, Mwl. Samweli Malechela alisema licha ya kuongeza mishahara na posho, Rais amelipa malimbikizo mengi ya mishahara kwa watumishi ndani ya mwezi uliopita. Katika Mkoa wa Dodoma, walimu zaidi ya 2,300 walipandishwa madaraja.
Mwl. Malechela aliongeza kuwa kupanda kwa mishahara na posho kutaimarisha na kuboresha uchumi wa watumishi pamoja na watanzania kwa ujumla. Mzunguko wa fedha utakua ni mkubwa jambo litakalopelekea uchumi wa Taifa kukua pia, aliongeza.
"Licha ya mambo yote ya kuboresha maslahi ya watumishi anayoyafanya Mama Rais wetu mpendwa lakini bado miradi mikubwa inaendelea kwa kasi ileile. Kwahiyo, ni dhahiri kabisa kuwa mama anaupiga mwingi. Hivyo, ni jukumu letu kumuunga mkono kwa kufanya kazi kwa juhudi kubwa ili kuendena na kauli ya kazi iendelee" alimalizia Mwl. Malechela.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.