Na. Dennis Gondwe, HOMBOLO BWAWANI
WAZAZI wa Shule ya Msingi Feza na jamii wamepongezwa kwa kuchangia watoto wenye mahita maalum kwa moyo na upendo sababu ni sehemu ya jamii jambo linalowapa faraja watoto.
Kauli hiyo ilitolewa na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Msingi Feza Dodoma, Mariam Mafuru alipokuwa akitoa salamu za shule hiyo kwa Jumuiya ya Shule ya Msingi Hombolo Bwawani alipoongoza ujumbe wa shule hiyo kupeleka zawadi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Kata ya Hombolo Bwawani.
Mafuru alisema “napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wazazi wenzangu tulioweza kushikiri na kujitoa kwa hali, mali na muda kuweza kuchangia zoezi hili na hatimae leo mafanikio yameonekana. Hiki kinachoonekana mbele yetu ni nguvu zetu sote, wazazi tumeshirikiana kwa pamoja tumeweka moyo na upendo kwa ajili ya kuwasaidia watoto wetu wapendwa. Kama familia ya Shule za Msingi Feza Dodoma tuna utaratibu wa kujumuika na wenzetu kwa kile kidogo ambacho Mwenyezi Mungu anakuwa ametubariki. Kwa mwaka huu tulifanya ‘Charity Marathon’ ambayo lengo kubwa ilikuwa kuelekeza kile kitakachopatikana kwa wale wenzetu wenye uhitaji maalum”.
Aidha, aliushukuru uongozi wa Shule ya Msingi Feza kwa kuwafanya wazazi sehemu ya kuisaidia jamii katika jambo jema. “Tunaomba tuendelee kushirikiana nao wasituache kwa sababu ni sehemu ya huduma. Tukumbuke kwamba tunao wale watoto wa kwetu, lakini hiki tulichokifanya ni kikubwa kuliko kile tunachokifanya kwa wale wa kwetu siku zote. Tutembee nao watoto ni taifa kubwa, watoto ni tegemezi sana na tunawategemea katika maendeleo ya taifa letu. Tuishi tukiwakumbuka, nashukuru sana kuwa sehemu ya hii familia” alisisitiza Mafuru.
Akiwasilisha taarifa fupi ya shule, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Hombolo Bwawani, Mwl. Pascal Ngoda alisema kuwa hiyo ni shule jumuishi ambayo inahusisha watoto wa kawaida na watoto wenye mahitaji maalum.
“Kutokana na jitihada za serikali na kutambua haki na usawa kwa watoto wenye mahitaji maalum mpaka sasa tuna watoto wenye mahitaji ya aina tano tofauti. Tuna watoto wenye ulemavu wa viungo, ambao tunashukuru wageni wetu wametuletea viti mwendo kwa ajili ya kuwasaidia kutembea kutoka bwenini hadi shuleni. Lakini pia watoto wenye ulemavu wa ngozi yaani Albino, lakini tuna watoto wenye changamoto ya akili. Tuna watoto wenye uono hafifu na tuna watoto wasioona kabisa. Msisite kututembelea, nyie ni sehemu ya faraja kwetu sisi, mnapokuja mara kwa mara hata bila chochote sisi tunawakaribisha na tunawapokea, tunatamani na tunajiona sisi ni sehemu ya jamii” alisema Mwl. Ngoda.
Akitoa shukrani, Diwani wa Kata ya Hombolo Bwawani, Ased Ndajiro alitoa shukrani kwa uongozi wa Shule ya Msingi Feza Dodoma kwa kuwapelekea zawadi wanafunzi wenye mahitaji maalum na kusema kuwa hiyo ni faraja kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Napenda kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan, Mbunge Anthony Mavunde. Sina budi kushukuru Shule ya Msingi Feza kwa kutuletea msaada wa viti mwendo na vifaa vitakavyowasaidia kwenye mwendo na kwenye masomo yao, kama mnavyowaona watoto wengine kunyanyuka ni shida. Nisisitize pia kwa yeyote anayewiwa na ana uwezo na nguvu hawa ni watu wanaohitaji mahitaji ya faraja, fedha, nguo na afya na mambo mengine ambayo mtu ataguswa nayo” alisema Ndajiro.
Ikumbukwe kuwa shule hiyo ilianza kama kituo cha watoto wenye ulemavu wa ngozi mwaka 1972.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.