Na. Aisha Ibrahim, DODOMA
WAFANYABIASHARA wanaojihusisha na kuuza vifaa vya shule kwa wanafunzi, wanaopatikana Mtaa wa One Way, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wamewaasa wazazi na walezi kujitokeza kununua vifaa hivyo kwa bei elekezi bila kuhofia, kwasababu mpaka sasa bei ni ya kawaida kama ilivyokuwa miezi iliyopita .
Hayo yalisemwa na baadhi ya wafanyabiashara wakieleza kuwa, bei ya vifaa vya shule kwa wanafunzi haijapanda kama walivyozoea misimu iliyopita hivyo, wazazi au walezi wajitokeze kwa wingi kununua vifaa vya shule kwa ajili ya watoto wao.
Noely Chibarabara alisema “bei zetu kwakweli hazijapanda, ziko palepale na hakuna shida yoyote ambayo imeweza kutokea kwamba tumepandisha bei, bei ipo palepale na bei zetu ni nzuri".
Akizungumzia kuhusu changamoto ya uzalishaji bidhaa viwandani kutokana na uhitaji mkubwa wa wateja, mfanyabiashara Paskali Faustine alisema bei inapanda msimu huu kutokana na uhitaji mkubwa wa bidhaa zitumikazo shuleni.
“Bei inapanda miezi hii kwa sababu ya uzalishaji viwandani unakuta ni changamoto, wanaotaka mahitaji ni wengi sana kwa sababu ni kipindi cha shule asilimia kubwa bidhaa zinakuwa ziko juu” alisema Faustine.
Akiongelea wafanyabiashara wanaopandisha bei katika msimu wa kuelekea shule kufunguliwa, mfanyabiashara Tonni Jamen aliwashauri kutokupandisha bei vifaa vya shule. Aidha, aliwashauri kuuza vifaa hivyo kwa bei elekezi ili kuwawezesha wazazi na walezi kumudu gharama na kuwashauri wasiogope kujitokeza kuwanunulia vifaa vya shule watoto wao ili waweze kwenda shule bila vikwazo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.