WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo amesema anatamani kuona Halmashauri nchini zinajitegemea zenyewe kupitia mapato ya ndani katika kipindi cha miaka mitatu ijayo na kwamba ifike muda ziwe zinalipa watumishi wake mishahara.
Waziri Jafo alitoa kauli hiyo Disemba 29, 2020 wakati alipotembelea ujenzi wa mradi wa 'Government City Complex' unaojengwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika eneo la Mji wa Serikali Mtumba unaogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 59.3 hadi kukamilika kwake ambapo ametumia nafasi hiyo kulipongeza jiji la Dodoma kwa kutekeleza mradi huo kwa kutumia mapato yake ya ndani na siyo fedha za Serikali Kuu.
Alisema hakuna Halmshauri yoyote iliyofanya uwekezaji mkubwa nchini kama uliofanyika katika Jiji la Dodoma huku akieleza kuwa sasa analiona jiji hilo kupitia viongozi wake kuwa wapo kwenye sura hiyo anayoitamani.
“Hakuna halmashauri yoyote iliyofanya uwekezaji mkubwa kama huu hivyo nawapongeza Jiji la Dodoma, nataka jengo hili liwe kielelezo na kama nilivyosema mimi matamanio yangu nataka nione halmashauri zinazoweza kujitegeme zenyewe ifike muda halmashauri iseme hata nikiwa na watumishi wangu nitawalipa mimi mwenyewe natamani itokee ndani ya miaka mitatu ijayo,” alisema Waziri huyo wa TAMISEMI.
Ameendelea kufafanua kuwa, analiona Jiji la Dodoma lipo kwenye ndoto zake za kuona Halmashauri zikijitegemea, kupitia hoteli hiyo kubwa itakayokuwa na kumbi kadhaa kubwa za mikutano iliyojengwa katika Mji wa Serikali, pamoja na hoteli nyingine ya Dodoma City Hotel yenye ghorofa 11 iliyojengwa na Jiji hilo na inatarajiwa kuanza kutumika wakati wowote kuanzia sasa ikiwa katikati ya Jiji hilo eneo la Paradise.
“Nikiiangalia hoteli kubwa iliyopo mjini ya ghorofa 11 (Dodoma City Hotel), nikiangalia soko lenu la Dodoma (Job Ndugai Market), nikiangalia eneo la maegesho ya magari Nala (Nala Lory Park), eneo la mapumziko na michezo Chinangali (Chinangali Recreational Park) na Kituo Kikuu cha Mabasi Dodoma, ninapata uhakika kwamba Halmashauri ya Jiji la Dodoma inaenda kujitegemea” alisisitiza Waziri Jafo.
Waziri ameutaka uongozi wa jiji la Dodoma kuhakikisha wanakwenda kusimamia kazi hiyo kwa kiwango cha juu ili iwe nzuri na ya mfano ambapo mtu akija ajifunze na kumtaka mkandarasi kutulia na kufanya kazi kwa uangalifu mkubwa, huku akimtaka kuongeza kasi ya ujenzi.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi wa Jiji hilo Joseph Mafuru alisema mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 59.3 kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza ni ujenzi wa jengo la 'Tower B' lenye ghorofa tano na kumbi tano za mikutano zenye uwezo wa kuchukua watu 1297.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.