WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Selemani Jafo ameipongeza Jumuiya ya Tawala za Mitaa nchini (ALAT) kwa kufanikiwa kujenga jengo la Ofisi zao jijini Dodoma.
Mhe. Jafo ametoa pongezi hizo leo jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa ofisi za Jumuiya hiyo na kusema wametii kwa vitendo agizo la Rais Dkt. John Magufuli la kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi.
Jengo hilo ambalo lilianza kujengwa Septemba 2018 limekamilika tayari kwa kuanza kutumika ambapo limegharimu kiasi cha Shilingi Milioni 121.3.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Jafo ameupongeza uongozi wa ALAT kwa ujenzi huo ambao umeacha historia kwani kabla ya hapo Jumuiya hiyo haikuwahi kumiliki ofisi zao wenyewe na badala yake walikua wamepanga.
"Nimeridhika na ujenzi wa jengo hili, hakika ni jengo zuri na thamani ya fedha imeonekana, Viongozi mliopo mtakumbukwa kwa hili ambalo mmelifanya. Mmefanya jambo la kihistoria na hii ndio maana ya uongozi ni alama.
Kwa muda mrefu ALAT ilikua ni kichaka cha watu kunufaisha matumbo yao lakini chini ya Mwenyekiti Gullamhafeez Mukadam Hafeez hata zile Halmashauri zilizokua haziipendi ALAT zitaanza kutoa michango bila kunung'unika," Amesema Mhe. Jafo.
Ameipongeza Jumuiya hiyo kwa namna ambavyo imekua ikisimamia miradi ya serikali za mitaa na kuahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana nao katika miradi mbalimbali ambayo imekua ikitekelezwa.
"Serikali za mitaa ndio utu wa mgongo wa Nchi yetu, tutaendelea kupeleka miradi mbalimbali ya kimaendeleo haswa kwenye afya na elimu na tunaamini hatua kubwa za kimaendeleo ya kiuchumi itapigwa kwa ushirikiano uliopo baina ya Serikali na ALAT," Amesema Mhe. Jafo.
Pia Waziri Jafo amezitaka Halmashauri zote nchini zinazodaiwa na Mabenki mikopo iliyokopwa na madiwani ziyalipe madeni hayo mara moja ili kuepusha Mabenki hayo kuzuia viinua mgongo vya madiwani pindi watakapomaliza muda wao.
"Nafahamu kuna halmashauri hazijalipa madeni ya madiwani wanayodaiwa benki baada ya madiwani wetu kukopa wakitegemea watakuwa wanakatwa kwenye posho zao za kila mwezi.
Ninawaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote zinazodaiwa zikiongozwa na halmashauri ya Gairo kulipa madeni hayo mara moja ili kuondoa usumbufu wa kuzuiliwa viinua mgongo vyao madiwani wetu hawa," Amesema Mhe Jafo.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa jengo hilo, Katibu Mkuu wa ALAT, Elirehema Kaaya amesema kukamilika kwa ujenzi wa jengo lao hilo kutaokoa kiasi cha Sh Milioni Tano kila mwezi walichokua wakitumia kama pango kwenye ofisi zao zilizopo jijini Dar es Salaam.
"Mhe Waziri ujenzi tumetumia takribani miaka miwili na tulijenga kwa fedha zetu wenyewe ambapo kiwanja pia kilikua ni chetu na mhandisi ni kutoka Jiji la Dodoma," Amesema Kaaya.
Nae Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Mhe Gulamhafeez Mukadam amesema malengo yao ni kujenga jengo refu la kitega uchumi ambalo litaongezea kipato kikubwa kitakachowawezesha kuzidi kujiendesha wenyewe.
"Tunaipongeza serikali ya awamu ya tano kwa miradi makubwa ya kimaendeleo inayotekelezwa kwenye serikali za mitaa hasa kwenye sekta ya Elimu, afya na miundombinu.
Lengo letu baada ya kukamilika kwa ujenzi huu ni kujenga jengo kubwa la kitega uchumi ili kuendana na Sera ya Rais Magufuli ya kukuza uchumi ambapo tunaamini licha ya kutupatia fedha nyingi litakua msaada pia kwa halmashauri zetu," Amesema Mukadam.
Chanzo: Tovuti ya tamisemi.go.tz
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.