Na. Aisha Ibrahim, DODOMA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa (Mb), aliwapongeza watumishi wa umma kwa kusimamia miradi mbalimbali jijini Dodoma ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aliyasema hayo katika Hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa Soko Kuu la Majengo pamoja ujenzi wa kituo cha daladala eneo la Mshikamano, Kizota na Nzuguni, iliyofanyika kiwanja cha Chinangali Park, Jijini Dodoma.
Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali Mohamed Mchengerwa, alitaka wakandarasi wote ambao hawajatekeleza majukumu yao katika miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa ujenzi wa barabara, kutopewa fursa ya kufanya kazi yoyote ikiwa ni onyo kwa wale wote wanaofanya kazi kwa uzembe na kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa wakati.
"Maelekezo yangu kwa mtendaji mkuu na katibu mkuu wa TARURA, Mkandarasi huyu asiruhusiwe kufanya kazi yoyote chini ya TARURA kuanzia sasa mpaka akamilishe mradi huu tunaoukusudia, pamoja na wengine ambao hawajakamilisha miradi hii ambayo ilipaswa ikamilike mwezi Februari, wasiruhusiwe kufanya kazi yoyote hata ya shilingi 500" alisema Mchengerwa.
Sambamba na hayo, alisisitiza kuwepo kwa utaratibu mzuri wa kuingia na kutoka katika eneo la Stesheni ya reli Jijini Dodoma ili wananchi na hata wageni kutoka nje ya Dodoma wajivunie uwepo wa Stesheni hiyo.
"Nawataka wakurugenzi wote wa majiji hasa Mkurungezi wa Jiji hili la Dodoma ambapo ni makao makuu ya nchi, mkuu wa Mkoa, Mkuu wa wilaya nendeni pale eneo la Stesheni ya reli na muweke utaratibu mzuri wa kuingia eneo hilo ili watanzania wanaokwenda na kurudi Jiji la Dodoma waweze kulifurahia jiji hili" alisema Mchengerwa.
Kwa upande wake Waziri wa madini, Anthony Mavunde (Mb) alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la
Dodoma ndiyo inayoongoza kwa mtandao mkubwa wa barabara zenye kiwango cha lami ambazo zina jumla ya urefu wa Kilomita 249.12 nchini Tanzania.
"Katika Halmashauri zote nchi nzima, Halmashauri ya Jiji la Dodoma ndiyo inaongoza kwa mtandao mrefu wa barabara za kiwango cha lami, sisi tuna Kilomita 249.12 ikifuatiwa na Halmashauri ya wilaya ya Kinondoni, wana urefu wa barabara wenye Kilomita 223" alisema Mavunde.
Aidha, aliendelea kwa kusema kuwa kumekuwa na kero mbalimbali katika vivuko vya maji katika maeneo ya Chaduru, Maili Mbili na Ntyuka ikiwemo wanafunzi kukwama na kushindwa kupita katika vivuko hivyo wakati wa mvua jambo linalopelekea kutofika shuleni kwa wakati.
"Vivuko hivi imekuwa ni kilio kikubwa, mvua inaponyesha watoto wanaotoka upande wa pili wamekuwa wakishindwa kuvuka lile Korongo na wamekuwa wakishindwa kwenda shule" alisema Mavunde.
Nae, Mtendaji mkuu, Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), Mhandisi Victor Seif, alisema lengo kuu la mradi wa "TACTIC" ni kuboresha usimamizi wa ukuaji wa miji pamoja na kuziwezesha Halmashauri za miji na majiji kutoa huduma bora kwa wananchi ikiwemo ujenzi wa miundombinu.
Alifafanua kuwa, kazi za ujenzi zinazofanyika katika mkataba wa "Package 1" ni Barabara ya Mbuyuni SP2 (Kilomita 1.69), Barabara ya Mauma-Makutano (Mita 760), Barabara ya Mbuyuni-Mwangaza (Kilomita 2.56), Barabara ya Ntyuka-Mkalama-Mapinduzi (Kilomita 5.2), Mtaro wa maji ya mvua Ilazo (Kilomita 2.1) na Uboreshaji wa mabwawa ya kuhifadhia maji ya mvua (3) na mitaro ya kutiririsha maji (Kilomita 2.81).
Lakini, aliongeza kuwa kazi za ujenzi zinazotarajiwa kufanyika katika Mkataba wa "Package 2 ni Uboreshaji wa Soko Kuu la Majengo pamoja na kituo cha daladala eneo la Mshikamano, Uboreshaji wa Stendi ya mabasi madogo eneo la Kizota, Uboreshaji eneo la mabasi madogo eneo la Nzuguni na Ujenzi wa Vivuko maji katika maeneo ya Chaduru, Mailimbili na Ntyuka.
Katika eneo la mabasi madogo (daladala) kutakuwa na maeneo matatu yaliyopangiwa kwaajili ya daladala kuruhusu urahisi wa kuingia na kutoka yenye makinga mvua au jua, taa za kutumia umeme jua, choo cha kulipia na eneo litakaloweza kupangwa wafanyabiashara.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.