Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekutana na Mawaziri na Makatibu wakuu kwenye eneo la tenki la maji la kutolea huduma kwenye ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba badala ya ukumbi wa Hazina kama ilivyokuwa imepangwa awali.
Akiwa kwenye kikao kazi hicho (site meeting) kilichohudhuriwa na mawaziri 15 na manaibu waziri wa wizara zao katika eneo la Mtumba umbali wa kilometa 17 kutoka jijini Dodoma, Waziri Mkuu amewaagiza Mawaziri wafike kwenye maeneo ya ujenzi wa ofisi zao, watathmini uwezo wa wakandarasi wanaojenga majengo ya wizara zao na pale watakapojiridhisha kuwa uwezo wao ni mdogo, wawabadilishe mara moja.
"Mawaziri mliopo na makatibu wakuu wote kaeni na wakandarasi wenu hapa site ili waeleze kazi hii itakamilishwa lini. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa kazi hii inakamilishwa kwa wakati" amesisitiza Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwapa mrejesho Mawaziri juu ya changamoto alizokutana nazo jana alipofanya ukaguzi wa ujenzi kwa kila wizara. "Nataka Mawaziri ambao wizara zao zinajengwa na watu wa Mzinga, wakae nao na kutathmini uwezo wao na kama mtaona hawawezi, mkabidhi kazi kwa mkandarasi mwingine" amesema.
Wakati huo huo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amemweleza Waziri Mkuu kwamba kuna wagongaji wa kokoto ambao wamepokea fedha lakini wakaamua kufunga machimbo yao kwa sababu ya sikukuu.
"Waziri wa Madini aongee nao hawa watu ili warejee na kufanya kazi kwa sababu baadhi yao wameshapokea fedha na mahitaji ya kokoto hapa ni makubwa na aliyebakia akifanya kazi ni Nyanza Road Works peke yake" alisema Waziri Lukuvi.
Naye Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani alimweleza Waziri Mkuu kwamba wizara yake imetoa 'transfoma' tisa za kusaidia kupoza umeme lakini ni wizara nne tu ndizo ambazo zimejitokeza na kulipia line za transfoma hizo.
"Wizara yetu tumetoa 'transfoma' tisa za kusaidia umeme upatikane eneo la ujenzi. Niwaombe mawaziri waliopo, walipie service line tu ambazo gharama yake ni shilingi 921,000 ili wafungiwe transfoma na kazi iweze kufanyika mchana na usiku. Hadi sasa, tumeshapokea maombi kutoka wizara nne tu za Maji, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera), Elimu na Nishati ili kazi imalizike ndani muda mfupi" alisema Waziri Kalemani.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi, alipotembelea ujenzi wa mradi wa ujenzi wa ofisi za wizara katika eneo la Mtumba nje kidogo ya Jiji la Dodoma ambapo ndipo panapojengwa Mji wa Serikali.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.