WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ipo imara na miradi yote ya kimkakati inaendelea kujengwa, hivyo Watanzania waendelee kuwa na imani na Serikali yao.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Jumanne, Aprili 20, 2021 baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni Kota, Dar es Salaam.
“Siri ya kuwepo mafanikio na maendeleo nchini ni utulivu na amani. Tulianza vizuri tangu Serikali ya Awamu ya kwanza, tutaendelea kuimarisha amani na utulivu.”
Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwaasa Watanzania watumie muda mwingi kufanya shughuli za maendeleo kuliko kufuatilia mambo mengine yasiyo ya tija.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Majaliwa amesema amefurahi kukuta majengo yamekamilika na kwamba ameridhika na maendeleo ya ujenzi wake.
Waziri mkuu ameuagiza uongozi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wahakikishe wanakamilisha kazi iliyosalia haraka ili mwaka huu wananchi waanze kuishi hapo.
Naye, Mtendaji Mkuu wa TBA, Daud Kondoro amesema mradi huo una jumla ya ‘block’ tano na ambazo zinauwezo wa kuchukua familia 656.
Amesema mbali na ujenzi wa nyumba hizo za makazi pia katika eneo hilo wanajenga maduka makubwa pamoja na vizimba kwa ajili ya wajasiliamali kufanya biashara.
Mradi ulianza kutekelezwa mwaka 2016 na unatarajiwa kukamilika Mei 2021. Hadi sasa umefikia asilimia 94 ya utekelezaji wake na gharama yake ni shilingi Bilioni 50.
Baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba za makazi za Magomeni Kota, Waziri Mkuu alikagua kituo cha Reli ya Kisasa cha Tanzanite jijini Dar es Salaam.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.