SERIKALI ya Tanzania imefadhili jumla ya miradi 215 ya Sayansi, Teknoljia na ubunifu katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, mifugo, afya, nishati, maliasili na viwanda kuanzia mwaka 2015, ambapo miradi 139 imekuwa ya utafiti, 47 ya kiubunifu, na 29 ya kuboresha miundombinu ya maabara za utafiti.
Hayo yamesemwa leo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kilele cha mashindano ya kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) mwaka 2021, yaliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri jijini hapa.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema kuwa mashindano hayo yana umuhimu mkubwa katika kuboresha uchumi wa nchi ambapo mashindano hayo yanagusa uchumi wa mtu binafsi na kuleta mafanikio ya kiuchumi kimataifa.
“Lakini vilevile, kwa upande wa mitaala kutoka ngazi mbalimbali za elimu ni vyema tuandae mitaala ya namna ambayo itawafanya wahitimu kuwa wabunifu mwisho wa masomo yao” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Akiongelea suala la hati miliki, Waziri Mkuu alisema kuwa, kazi kubwa ni kutoa kipaumbele kwa hati miliki ya mgunduzi kwa sababu ndiyo njia ya kumfanya apate faida kupitia ubunifu wake.
“Takwimu zetu zinaonesha kuwa shirika la hati miliki duniani linaitwa ‘World Intellectual Property Organisation’ (WIPO), linalokusanya maombi ya hati miliki kutoka nchi mbalimbali na mpaka kufikia mwaka 2020 Tanzania tulipeleka maombi nane huku nchi za jirani 372, Afrika ya Kusini 1,514” alisema Waziri Mkuu.
Aidha, alizishukuru taasisi 50 zikiwemo za Serikali na zisizo za Serikali zilizoshiriki katika mashindano ya kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, na kuongeza kuwa changamoto zilizopo zimekwisha elekezwa kwa Wizara na taasisi zenye dhamana.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, yamefanyika kwa mara ya tatu katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma yakiongozwa na kaulimbiu isemayo “Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa Uchumi endelevu”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.