WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa jana amekutana kwa mazungumzo na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF), Bilionea Patrice Motsepe ofisini kwake Mlimwa hapa Jijini Dodoma na kujadiliana naye masuala muhimu ya kuendeleza michezo nchini.
Motsepe, raia wa Afrika Kusini na mmiliki wa klabu ya Mamelod Sundows yupo nchini kwa mwaliko wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia na leo anatarajiwa kuhudhuria fainali ya Kombe la Kagame kati ya Expresa ya Uganda na Nyasa Big Bullets ya Malawi mchezo utakaochezwa katika dimba la Benjamin Mkapa kuanzia saa 1 kamili usiku Jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu alimweleza mikakati ambayo Serikali inatumia ili kuinua kiwango cha soka nchini. "Sisi tumeanza kuboresha michezo nchini chini ya mpango unaohusisha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mpango huu unalenga kuibua vipaji vya vijana kupitia mashindano ua UMITASHUMTA, UMISETA, Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati." Alisema.
Katika mazungumzo yao, walijadiliana suala la kuendelea kutenga bajeti ya kuinua michezo kwa vile nchi nyingi zinashindwa kufanya vizuri kwenye michezo kwa sababu hazitengi bajeti. "Nimemweleza kuwa hapa kwetu kupitia Bunge letu tukufu, tumekuwa tukitenga bajeti hiyo japokuwa tunajua kuwa haitoshelezi mahitaji yote.
Kuhusu uendelezaji wa michezo nchini, Rais wa CAF ametusihi tuwe na mpango madhubuti wa kupata maeneo ya kufanyia mazoezi, tuwe na viwanja bora vyenye vipimo vya kisasa, jambo ambalo nimemweleza linatekelezwa na shirikisho la soka nchini. Pili, ametutaka tuandae vijana kuanzia umri mdogo, tuwe na taasisi za Serikali na za sekta binafsi zinazofundisha soka, waamuzi na makocha ili tuwaibue akina Samatta wengi zaidi kwani na sisi tunaamini kuwa wapo."
Naye Dkt. Motsepe amesema katika uongozi wake amelenga mambo makuu matatu ambayo ni sekta binafsi kuwekeza kwenye michezo na kuongeza udhamini, ujenzi wa vituo vya michezo na vituo vya kuendeleza vijana.
Amesema chini ya mfuko wa dola bilioni mona amedhamiria kuimarisha miundombinu ya michezo. Kuna baadhi ya nchi za Afrika zina viwanja vikubwa vya micjezo lakini havijakidhi vigezo vya FIFA. Tunataka na wao wafikie viwango vya kimataifa.
Motsepe amesifu kuwa timu ya Taifa ya Tanzania ina uwezo kuwa timu bingwa barani Afrika kutokana na umahiri walionao hivi sasa na ametumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuunga mkono michezo nchini ambapo wiki ijayo atapokea kombe la CECAFA - 2021 la vijana wenye umri chini ya miaka 23.
Kiongozi huyo wa shirikisho la mpira Afrika ameipongeza Tanzania kwa kuwa nchi ya kuigwa kutokana na wananchi wake wengi kupenda michezo na hasa kunapokuwa na mechi zinazokutanisha vilabu vikubwa nchini kwa vile zinawaleta mashabiki hata kutoka nchi jirani.
Ikumbukwe Jiji la Dodoma linamiliki timu ya Dodoma Jiji FC inayoshiriki katika ligi kuu hapa nchini Tanzania.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.