WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa jitihada kubwa zilizofanyika kwa ajili ya kutokomeza ugonjwa wa Malaria.
Waziri Ummy ametoa pongezi hizo leo wakati alipokuwa anagawa vyandarua vyenye dawa kwa akinamama wajawazito na wenye watoto wadogo katika kituo cha Afya cha Makole Jijini Dodoma.
Waziri Ummy amesema Halmashauri ya Jiji la Dodoma imetokomeza ugonjwa wa Malaria kutoka asilimia 1 mpaka asilimia 0.6 ikiwa ni mafanikio makubwa, ambapo amesema katika kipindi cha miaka mitatu nchi nzima ugonjwa wa Malaria umeweza kupungua kutoka asilimia 14 mwaka 2015 mpaka asilimia 7 mwaka 2018.
"Toka Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Mhe. John Magufuli iingie madarakani tumeweza kutekeleza mikakati mbalimbali ya kutokomeza Malaria nchini, katika kipindi kifupi cha miaka mitatu tumeweza kupunguza Malaria zaidi ya asilimia 50 kutoka asilimia 14 mwaka 2015 mpaka asilimia 7 mwaka 2018", alisema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy aliwasifu akinababa walioleta watoto wao kliniki katika kituo hicho na amewataka wananchi kwa ujumla kutimiza wajibu wao ili kutokomeza Malaria kama kauli mbiu ya mwaka huu inavyosema "Ziro Malaria inaanza na mimi", hivyo amewataka wakina mama wajawazito kuhudhuria kliniki kwa ajili ya uchunguzi wa afya zao na kufanyiwa vipimo vyote kikiwemo cha Malaria.
Waziri huyo alibainisha kuwa, Tanzania bado haijafanya vizuri katika takwimu za akina mama wajawazito kuhudhuria kliniki ambapo katika akinamama wajawazito 100 ni akinamama 29 ndiyo wanaohudhuria kliniki mara nne katika kipindi cha ujauzito.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa ambaye pia ni Mratibu wa Malaria wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Francis Bujiku alisema mafanikio ya kutokomeza Malaria katika jiji la Dodoma yamekuja baada ya utekelezaji wa afua mbalimbali za Malaria ikiwa ni pamoja na kuhakikisha tiba sahihi za Malaria zinazotolewa katika vituo vyote vya afya, elimu ya kujikinga na ugonjwa huo, pamoja na Mkoa kufanikiwa kuangamiza viluilui wa mbu kwa kunyunyizia dawa kwenye mazalia yao.
Bujiku alisema mwaka 2015 Mkoa uliendesha zoezi la ugawaji vyandarua vyenye dawa kwenye ngazi ya kaya, ambapo takribani vyandarua milioni moja na laki tano viligawiwa kwa wananchi, huku akina mama wajawazito waliofika kliniki kwenye hudhurio la kwanza la ujauzito na watoto chini ya mwaka mmoja waliofika kupata chanjo ya surua nao wakipewa vyandarua hivyo.
Waziri Ummy Mwalimu akimuangalia mtoto aliyeletwa kliniki ya Kituo cha Afya Makole kilichopo Jijini Dodoma
kwa ajili ya kupata chanjo wakati alipotembelea kituo hicho na kugawa vyandarua vyenye dawa kwa
wanawake wajawazito na watoto walio na umri chini ya mwaka mmoja.
Waziri Ummy Mwalimu akimpongeza baba aliyeleta mtoto kliniki kwa ajili ya kupata chanjo katika kituo cha
Afya Makole Jijini Dodoma.
Waziri Ummy Mwalimu akiwa na baadhi ya akinamama waliopewa vyandarua baada ya kufika kliniki katika
kituo cha Afya cha Makole Jijini Dodoma wakati Waziri alipofika na kugawa vyandarua hivyo.
Chanzo: afyablog.moh.go.tz (afyablog.moh.go.tz)
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.