Na. Dennis Gondwe, MAKOLE
MIAKA 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara Wilaya ya Dodoma imewapatia zawadi kina mama waliojifungua katika Kituo cha Afya Makole na kuwatakia heri na kuwahakikishia kuwa serikali inataendelea kutoa huduma bora kwao.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alipoongoza timu ya wataalam wa wilaya na halmashauri kukagua hali ya huduma katika Kituo cha Afya Makole, kutembelea kina mama wanaotarajia kujifungua na waliojifungua na kuwapatia zawadi mbalimbali.
Alhaj Shekimweri alisema kuwa Wilaya ya Dodoma katika kuelekea maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara imetembelea Kituo cha Afya Makole kukagua hali ya utoaji huduma. “Kwa niaba ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan tumekuja kuona huduma zinatolewaje hapa sehemu ya kujifungulia. Tunafahamu hapa kuna wastani wa kujifungua kawaida wanawake kati ya 15-25 kwa siku na wale wanaojifungua kwa upasuaji ni kati ya 4-6 kwa siku. Hii ni idadi kubwa hivyo, tuna hamu ya kupata mrejesho wa huduma hizo. Lakini pia kuwaletea zawadi ndogo ya kuadhimisha miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania bara tukiamini kuwa uhuru huu siyo tu wa kujitawala lakini wa kujiletea maendeleo. Kina mama wajawazito kupata huduma nzuri za kliniki wakielekea kujifungua, wajifungue katika maeneo salama katika vituo vya kutolea huduma kama hapa Kituo cha Afya Makole. Na haya ndiyo matunda ya uhuru wetu” alisema Alhaj Shekimweri.
Alisema kuwa Rais, amefanya mambo makubwa katika sekta ya Afya. “Mheshimiwa Rais, anatujengea hospitali ya wilaya, tayari ametuletea shilingi 1,500,000,000 za kujenga hospitali hiyo na hapa Makole ametuletea shilingi 750 za kuboresha huduma za Afya. Tumekuja kuwasalimia na tunaendelea kuwaombea heri kwa Mungu na tunawapenda na tunawathamini na tupo hapa kuonesha upendo huo” alisema Alhaj Shekimweri.
Akitoa taarifa fupi ya huduma kwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method alisema kuwa watu wengi wanapenda kujifungua katika Kituo cha Afya Makole kutoka na ubora wa huduma. “Tumekuwa tukipata kina mama takribani 20 wanaojifungua kila siku katika kituo hiki. Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya kama ulivyoona kuna kimama takribani 47 waliolazwa na waliojifungua katika kituo hiki. Tunashukuru tunapopata matokeo kuwa wanajifungua salama ndiyo dhamira ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona kina mama wanajifungua salama lakini na watoto wao wakiwa salama” alisema Dkt. Method.
Kwa upande wa mama aliyejifungua katika kituo hicho, Stella Gilbert alisema huduma ni nzuri. “Nimejifungua leo saa sita mchana katika Kituo cha Afya Makole tena nimejifungua salama mtoto wa kiume. Nawashukuru madaktari na wauguzi wanahudumia vizuri na wanajali sana wagonjwa, Mungu awabariki sana. Hali ya huduma ni nzuri sana” alisema Gilbert.
Katika kuelekea miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Wilaya ya Dodoma ilitembelea Kituo cha Afya Makole kukagua hali ya utoaji huduma katika wodi ya kima mama, kuwatia moyo kina mama wanaotarajia kujifungua na waliojifungua na kuwapatia zawadi mbalimbali.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.