MKURUGENZI Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Bw. Rashid Mafutaa ametoa wito kwa watoa huduma za afya kushirikiana na wadau wa mashirika yanayotoa huduma kwa watu wenye ulemavu nchini kuimarisha huduma za utambuzi wa mapema kwa watoto wenye ulemavu katika jamii na vituo vya afya.
Bw. Mafutaa ameyasema hayo mapema wiki hii alipokuwa akifungua kikao kazi cha kutengeneza mpango mkakati wa taifa wa utengemao (National Rehabilitation Strategic Plan-NRSP) jijini Dodoma.
“Mhe. Rais alisisitiza katika kikao chake na watu wenye ulemavu kuimarisha suala la utambuzi wa mapema kwa watoto wenye ulemavu katika jamii vilevile katika vituo vya kutolea huduma za afya” alisema Bw. Mafutaa na kuwataka wataalam kutengeneza Muongozo ambao utaenda kutusaidia katika uimarishaji wa masuala ya utambuzi wa mapema kwa watoto wenye ulemavu katika jamii
Mkurugenzi huyo aliendelea kusisitiza kuwa endapo jamii itawahi mapema kumgundua mtoto mwenye tatizo la ulemavu itasadia pia katika kuwahi kumuweka kwenye matibabu na kupunguza athari ya kiungo kilichopata changamoto hiyo na kurejea katika hali yake ya kawaida na kumfanya muhusika kujimudu na kuendelea na shughuli zake za kila siku kama kawaida.
“Mfano kama mtu ana changamoto ya usikivu naamini ukimuwahi mapema kumgundua na akapata huduma za mapema atakuwa katika nafasi nzuri ya kuweza kupata usikivu wa awali na kurudi katika hali yake ya kawaida na kuendelea na shughuli zake” alifafanua Bw. Mafutaa
Aidha, Mkurugenzi Mafutaa aliwataka wadau kuungana pamoja katika kuunga mkono jitihada mbambali za serikali za utambuzi wa mapema kwa watoto wenye ulemavu na kuelekeza nguvu ya pamoja katika kutengeneza mpango mkakati wa utengemao ambao utasaidia kufanya utetezi kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum sambamba na kuchochea kuboresha sera na kutekeleza huduma zinazohusu utengemao.
"Tunawashukuru Shirika la Blind Mission (CBM) kwa kufadhili mkutano huu muhimu kama wadau kwa watu wenye ulemavu nchini".
Chanzo: wizara_afyatz (instagram)
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.