Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma na jiji la Linz la nchini Austria zimesaini hati ya makubaliano (Memorandum of Understanding) ya
ushirikiano katika nyanja za Utunzaji wa Mazingira, kuimarisha huduma za kijamii, uwekezaji wa kibiashara, kuimarisha miundombinu na
teknolojia, na kuimarisha huduma ya kupambana na majanga ya moto na uokozi.
Maeneo mengine ambayo mamlaka hizo mbili zimekubaliana kushirikiana ni pamoja kutoa mafunzo mbalimbali wa watumishi wake na
Madiwani wa pande zote mbili, kubadilishana watumishi pamoja na kushirikiana katika jambo lolote litakaloonekana kuwa na manufaa kwa
wananchi wa pande zote.
Makubaliano hayo yalifikiwa hivi karibuni wakati wa ziara ya siku moja ya Naibu Meya wa jiji la Linz Detlef Wimmer na ujumbe wake katika
Manispaa ya Dodoma ambapo alitembelea maeneo kadhaa ikiwemo Dampo la kisasa la takataka lililopo katika kijiji cha Chidaya kata ya Ntyuka
Manispaa ya Dodoma na shamba la zabibu katika kata ya Mtumba ili kuangalia fursa za uwekezaji katika sekta ya kilimo.
Akisaini makubaliano hayo kwa niaba ya Manispaa ya Dodoma, Meya wa Manispaa hiyo Mstahiki Jaffar Mwanyemba alisema ushirikiano huo
umekuja wakati muafaka na kwamba utakuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wa miji hiyo huku akitoa wito kwa marafiki na wawekezaji
wengine kujitokeza kwani mji wa Dodoma kwa sasa umefunguka na kwamba ni wakati muafaka wa kuwekeza Dodoma.
Kwa upande wake Naibu Meya wa jiji la Linz Detlef Wimmer ambaye alisaini hati hiyo kwa niaba ya mamlaka ya jiji hilo alielezea kuvutiwa
kwake na mji wa Dodoma na kwamba amejifunza mengi katika ziara yake huku akiahidi ushirikiano wa dhati katika maeneo waliyokubaliana.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi alisema ushirikiano kati ya Manispaa ya Dodoma na Jiji la Linz ni mwanzo tu wa
juhudi zinazofanywa na Manispaa katika kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji mbalimbali ili kuhakikisha Manispaa hiyo inakua kwa kasi
huku huduma za kijamii zikipewa kipaumbele kwa manufaa ya wakazi wake na hata wa mikoa ya jirani.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.