MAELEZO MAFUPI YA IDARA YA MAZINGIRA NA UDHIBITI WA TAKA NGUMU KATIKA JIJI LA DODOMA
UTANGULIZI
Halmashauri ya Jiji ya Dodoma ni miongoni mwa Halmashauri nane za Mkoa wa Dodoma. Halmashauri hii ilianzishwa mwaka 1973 na Mwaka 1980 ilipewa hadhi ya kuwa Manispaa na kisha tarehe 26 Aprili, 2018 kupandishwa hadhi ya kuwa Jiji. Kiutawala Halmashauri ina jumla ya tarafa 4 ambazo ni Zuzu, Hombolo, Kikombo na Dodoma Mjini. Kuna Kata 41, Vijiji 18, Mitaa 170 na Vitongoji 88.
Usafi wa mazingira ni mojawapo ya eneo nyeti linalotiliwa mkazo na serikali ya awamu ya tano, sifa na heshima ya mji wowote duniani inaanza kwenye masuala ya usafi. Usafi wa mazingira huvutia wageni mbalimbali ndani na nje ya nchi, hali ambayo huchangia kuongezeka kwa mapato pia kupelekea kuepusha magonjwa ya mlipuko na magonjwa ya kuambukiza kama vile kipindupindu na magonjwa ya kuhara.
Uhifadhi na utunzaji wa mazingira Unahusisha usimamizi wa shughuli zote zinazopelekea uharibifu wa mazingira ikiwemo miradi mbalimbali na shughuli binafisi. Pia kitengo cha mazingira kinashughulika na kutoa maelekezo kwa wawekezaji kuhusu ufanyikaji wa tathimini ya athari kwa mazingira (EIA) kabla ya mradi kuanza, kutembelea na kukagua maeneo ya miradi, kupitia na kuhakiki ripoti za tathmini za athari ya mazingira za miradi mbalimbali, pamoja na kufanya tathimini ya athari ya mazingira kwa ajili ya miradi midogo isiyo na athari kubwa katika ngazi ya Halmashauri.
Kazi/Majukumu yanayopaswa kutekelezwa na Idara ya Mazingira na Udhibiti wa taka ngumu ni pamoja na :-
Shughuli za Usafishaji:
1. Usafishaji wa majengo, maeneo ya wazi, mifereji na barabara.
2. Utunzaji, uchambuzi na usafirishaji wa taka.
3. Uchambuzi , utupaji wa taka na uendeshaji wa dampo la kisasa.
Shughuli za Mazingira
1. Udhibiti wa uchafuzi wa mazingira, maji, hewa na sauti.
2. Utunzaji wa mazingira na upandaji wa miti na upendezeshaji wa mazingira.
3. Kufanya tathmini ya athari za mazingira/ Environmental Impact Assessment (EIA).
SEKTA YA MAZINGIRA/MALIASILI NA UTALII
Uoto wa Asili
Uoto wa Asili wa Jiji ya Dodoma ni ukanda wa savanna ambao umejaa vichaka vyenye miti yenye miiba na misitu michache ambayo inaendelea kupungua kila wakati kwa sababu ya ongezeko la haraka la idadi ya watu linalopelekea mabadiliko ya matumizi ya ardhi (Land use cover change.). Aina ya miti inayopatikana ni pamoja na mibuyu (adonsonia, digitata), mikababu, (acacia albida), mikungungu, (acacia tottolis na albizia lebbeck) mijohoro (acacia siamea) mlonge (moringa oleifera) Miti ya x-mass (delonix elera) miarobaini (azadirachtaindica) Mikwaju (Tamarindus indica) miembe (mangifera indica) Euphobia tricholor, ficu spp, na Mitopetope (Leucaenia leucocephala).
Nishati
Zaidi ya 85% ya wakazi wa Jiji ya Dodoma wanategemea nishati ya kuni na mkaa kwa matumizi ya nyumbani na kwenye taasisi mbalimbali kama vile mashuleni na katika magereza. Utegemezi huu uliokithiri umekuwa chanzo kikubwa cha upotevu wa misitu katika Jiji ya Dodoma. Maeneo ya vijijini yanategemea zaidi kuni wakati maeneo ya mjini wanategemea mkaa. Kwa kulinganisha na familia za Jiji 87,474 familia moja inatumia magunia 2.25 ya mkaa kwa mwezi na kufanya matumizi kwa mwaka kufikia magunia ya mkaa 196,817. Nishati nyingine inayotumika ingawa ni kwa kiwango kidogo ni gesi asilia, umeme, umeme jua na umeme upepo.
Misitu
Jiji ya Dodoma imezungukwa na misitu ya hifadhi mfano Kinyami yenye ukubwa wa hekta 43330, Dodoma reservoir 455.2, Chigongwe hekta 4522.7, Mahomanyika hekta 4000, Nzuguni hekta 800 na Bihawana hekta 4000.
Aidha Halmashauri ya Jiji la Dodoma inamiliki vitalu viwili vya miche vyenye jumla ya miche 60,000 ambapo kitalu cha Arusha Road Nursery kina miche 40,000 na kitalu cha Hado Mailimbili miche 20,000.
Wanyamapori
Tofauti na Halmashauri zingine Halmashauri ya Manipaa ya Dodoma haina rasilimali za wanyama pori kwa sababu mfumo wa ikolojia wa Halmashauri haustawishi wanyamapori ingawa kuna ushoroba katika maeneo machache ambao wanyama wanapita wanapohama kutoka pori la Swagaswaga Kondoa kuelekea pori la Ruaha mkoa wa Iringa. Baadhi ya wanyamapori wanaopatikana ni Tembo, Kiboko, Chui, Fisi, Digidigi, Nyani, na aina za ndege kama jamii ya finches wanaopatikana mtaa wa Mapinduzi.
Madini
Katika Halmashauri ya Jiji ya Dodoma hakuna machimbo makubwa ya madini ingawa kuna dalili za upatikanaji wa dhahabu katika eneo la Nzuguni na madini ya Galena huko Hombolo. Madini inayopatikana kwa wingi ni Madini ujenzi yaani mchanga, kokoto, mawe, udongo mwekundu na kifusi. Uvunaji wa madini haya ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira japo kwa upande mwingine kimekuwa chanzo cha mapato ya Halmashauri.
Halmashauri imetenga maeneo ya makorongo ya asili kwa ajili ya uvunaji mchanga. Kulingana na uhitaji wa madini hayo kwenye shughuli za kimaendeleo mchanga umepungua sana makorongoni na kusababisha wawekezaji kuchimba mchanga mashambani na kutengeneza makorongo makubwa katika maeneo mbalimmbali ya mashamba.
UDHIBITI WA TAKA NGUMU 2017/2018
Hali ya udhibiti taka ngumu na usafi wa Mazingira katika Jiji imeimarika, aidha Jiji ya Dodoma inakisiwa kuzalisha tani 350 za taka ngumu kwa siku ambapo kata za nje ya mji uzalishaji tani 114 na Kata za mjini uzalisha ni tani 236. Aidha wastani wa tani 150 tu ndiyo zinaondoshwa mjini kwa siku sawa na asilimia 66%, hali hiyo imekuwa ikichangiwa na uhaba mkubwa wa vifaa hasa Skip bucket kwani kwa sasa zipo 61 kati ya 187 zinazohitajika kwa sasa kwa mujibu wa mwongozo.
Kwa sasa; Halmashauri inashirikiana na kampuni ya uzoaji taka; Green Waste Pro kwa Kata nane za mjini utoaji wa huduma ya kuzoa taka na kusafisha mji. Uzoaji wa taka katika maeneo mbalimbali ya mji, vikundi vya kijamii vimekuwa vinatoa huduma ya kuzoa taka katika ngazi ya kaya, na maeneo mbalimbali ya biashara na kupeleka katika vituo vya kupokelea taka (collection point) ambapo kuna makasha ya kupokelea taka (Skip buckets). Halmashauri inasafirisha taka mpaka kwenye dampo la kisasa lililoko eneo la Chidaya Kata ya Matumbulu.
Dampo la Kisasa la Chidaya
Dampo la Kisasa la Chidaya lina Ukubwa wa Hekari 48 ambapo eneo linalotumika kwa sasa lina Ukubwa wa Hekari 10. Dampo hili lina uwezo wa kutumika kwa muda wa miaka 18 hadi 20. Dampo hili linapokea taka kila siku kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 12 jioni. Taka hupimwa katika mizani iliyopo katika geti la kuingilia dampo ili kujua uzito wake kwa kila gari inayoleta taka Dampo na kutunza takwimu. Taka zilizomwagwa husukumwa, husambazwa hushindiliwa na hufunikwa na kifusi cha udongo kila siku.Wastani wa tani 120 -150 za taka ngumu hutupwa katika Dampo kila siku kutoka katika vyanzo mbalimbali vya uzalishaji taka.
Mipango ya Baadaye ya Kuteketeza Taka
• Kuhamasisha wadau wa miradi mbalimbali ya urejelezaji wa taka mfano utengenezaji wa mbolea ya mboji kutokana na taka zinazo oza (organic waste) na utengenezaji nishati mbalimbali kwa kutumia taka kama malighafi.
• Kubinafsisha huduma ya ukusanyaji taka
• Baada ya awamu ya kwanza ya dampo kujaa kuna uwezekano wa kuvuna gesi na kuna uwezekano wa kuzalisha umeme.
• Kuanzisha kituo cha kuchakata taka kabla ya kufukia (MRF-Material Recovery Facility). Kituo cha aina hii kinatoa fursa ya kuchepusha aina ya taka ambazo zinaweza kurejelezwa tena kama malighafi katika viwanda.
• Jiji ya Dodoma ina fursa kubwa ya kuanza kutekeleza mpango wa kupunguza kiasi cha taka kinachozolewa, kusafirishwa na kutupwa katika Dampo la Chidaya. Katika mzingo wa mjumuisho wa uzalishaji wa taka (waste composition) kuna fursa za aina mbalimbali ambazo huzalishwa Jiji na zinaweza kurejelezwa tena.
Faida za Mkakati wa Kupunguza Taka
• Kupunguza gharama za usafirishaji taka hadi dampo.
• Kupungua kwa gharama za udhibiti taka katika dampo.
• Dampo kutumika kwa muda mrefu zaidi bila kujaa haraka
• Kutoa ajira kwa vijana na akina mama katika kuchambua taka zenye thamani na kuzijereza tena na kupata malighafi zitokanazo na taka ngumu,
• Mazao ya shamba yataweza kustawi zaidi kutokana na mbolea mboji inayoweza kuzalishwa kutokana na taka zinazoweza oza (organic waste),
Changamoto na Mikakati
Changamoto
Halmashauri ya Jiji inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo;
• Kuongezeka kwa uzalishaji wa taka ngumu uliotokana na ongezeko la watu katika Halmashauri ya Jiji ya Dodoma baada ya serikali kuhamia Dodoma.
• Kutokuwepo na mfumo mzima wa uchambuzi wa taka (sorting)
• Uharibifu waArdhi kutoka na na kilimo na uchimbaji wa mchanga
• Ukataji miti hovyo na uharibifu wa misitu kwa sababu ya utegemezi wa wakazi kwenye nishati ya kuni na mkaa.
Mikakati
Mikakati ya kutatua changamoto zilizopo katika Halmashauri ni kama ifuatavyo: -
• Kuimarisha usimamizi na udhibiti wa uchafuzi wa mazingira katika ngazi ya Kaya, Mitaa na maeneo ya biashara katika Jiji kwa 80 % ifikapo mwaka 2018.
• Kuimarisha ugatuzi wa usimamizi wa huduma ya usafi na udhibiti wa taka ngumu katika ngazi ya Kata.
• Kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo katika suala la Usafi wa Jiji na Uondoshaji wa taka ngumu hasa katika kubinafsisha baadhi ya kata .
• Kutenga bajeti ya ununuzi wa vifaa vya kutunzia na kuhifadhia taka katika mwaka wa fedha 2018/2019
• Kuimarisha usimamizi wa sheria ndogo na kufanya doria za Mara kwa mara katika maeneo ya Uvunaji wa madini ujenzi na misitu inayohifadhiwa na Jiji .
• Kutekeleza agizo la serikali la kufanya usafi kila jumamosi ya mwisho wa mwezi na agizo la Mhe Mkuu wa Mkoa wa Dodoma la kufanya usafi kila jumamosi.
• Kuendelea kuelimisha wananchi na wadau mbalimbali juu ya umuhimu na wajibu wa kila mdau katika kuhakikisha anatunza mazingira na kufanya usafi mita tano kuzunguka eneo lake la biashara na Mkazi ndani ya Jiji la Dodoma
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.