HISTORIA YA MANISPAA YA DODOMA
Miaka mingi iliyopita mji huu ambao unaitwa Dodoma ulikuwa ukifahamika kama Calangu (Chalangu) mji huu haukuwa na wenyeji bali ulikuwa na wahamiaji toka maeneo mengine ambao ni wamanghala, wabambali, wayenzele na wanghulimba. Wahamiaji hawa walikuwa wakitofautiana kwa tabia zao, wamanghala na wabambali waliishi msituni na walikuwa wawindaji wakila nyama na asali. Na wayenzele na wa wanghulimba walikuwa wakulima na wafugaji. Watu hawa walikuwa waoga kiasili hivyo watu wengine walipoanza kuingia kutoka maeneo ya kaskazini wambugwe, magharibi wanyamwezi na kusini wa hehe watu hawa waliondoka na kwenda kuishi sehemu nyingine.
Sababu ya wahamiaji hawa kuitwa wagogo, inatokana na wafanyabiashara wakinyamwezi walipokuwa wakipita na bidhaaa zao kuelekea Pwani kwa biashara, walipofika kati ya Itigi na Manyoni walikuta mti mkubwa umeanguka na kuzuia njia, hivyo kwa muda mrefu wali lazimika kulala upande mmoja kabla ya kuvukia upande wa pili wa mti (gogo). Hii iliwafanya kila walipoulizwa wanalala wapi kabla ya kuendelea na safari walisema wanalala kwenye limgogo. Kwa hiyo wahamiaji hawa wakafahamika kama gogo (wagogo) kutokana na gogo hilo. Mnamo mwaka 1912 alifika mjerumani Dr. Spreling (Spelenje), na kuanzisha ngome yake, ngome hiyo kwa sasa ni ofisi ya Waziri Mkuu. Ofisi aliyokuwa akifanyia kazi za utawala na utoaji maamuzi kwa wahalifu (kufungwa, kuchapwa viboko na kunyongwa) kwa sasa ni Ofisi ya CCM Wilaya ya Dodoma Mjini. Bustani aliyopenda kutembelea na kupumzika ilikuwa eneo la Kikuyu ambayo kwa sasa ni Chuo Kikuu cha St. John’s, eneo hili kwa wakati huo lilikuwa tepetepe na mapitio ya wanyama watokao mbuga za kaskazini (Arusha) kuelekea mbuga za kusini (Mikumi). Mapitio ya wanyama hao ndio yaliyosababisha kubadilika kwa jina la eneo hili baada ya tembo kudidimia katika eneo hilo tepetepe karibu na shule ya sekondari mazengo ambayo sasa ni chuo kikuu cha St. Johns. Tendo hili la kudidimia kwa lugha ya Kigogo linajulikana kama IDODOMIA hivyo baada ya kitendo hiki jina likabadilika kutoka Calangu (Chalangu) nakuwa Idodomia (DODOMA).Mji wa Dodoma ulitangazwa rasmi kuwa makao makuu ya Chama na Serikali chini ya kifungu cha sheria No.320 ya mwaka 1973. Baada ya hapo matukio ya mafanikio yalifuata. Mwaka 1980 mji wa Dodoma ulipewa hadhi ya kuwa Manispaa. Mwaka 1995 serikali iliamua kuwa shughuli zote za bunge zifanyikie Dodoma. Bunge lilianza shughuli zake rasmi mwezi Februari 1996.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.