Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa mnamo tarehe 26 Aprili, 1964 kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (inayojumuisha Visiwa vya Pemba na Unguja). Tanganyika ilikuwa ni mwendelezo wa koloni la Ujerumani, utawala wa Waingereza kwa Mamlaka ya Umoja wa Mataifa, Himaya ya Umoja wa Mataifa chini ya utawala wa Uingereza na mwisho Taifa huru kuanzia mwaka 1961 ndani ya nchi za Jumuiya ya Madola. Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ziliingia mkataba wa Muungano mnamo mwaka 1964 na kuanzishwa Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Aprili 22, 1964 huko Zanzibar.
Mkataba huo ulithibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi hapo tarehe 26 Aprili, 1964. Tarehe 27 Aprili, 1964, viongozi wa nchi zote mbili walikutana katika ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam na kubadilishana Hati za Muungano.
Sheria za Muungano zilitoa tamko la Jamhuri ya Muungano katika Ibara ya 4 kwamba: “Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zitalazimika, baada ya kuungana na siku zote baada ya kuungana, kuunganishwa kuwa Dola ya Jamhuri kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar’ (Ibara ya 4 Sheria za Muungano) Jina hili la “Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar” lilibadilishwa baadae mnamo tarehe 28 Oktoba, 1964 na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia Sheria ya Jamhuri ya Muungano, Sheria namba 61 ya mwaka 1964.
Muundo wa Muungano
Muundo wa Muungano wa Tanzania kama ulivyoelezwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, una vyombo viwili vyenye mamlaka 3 ya utendaji ambavyo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji haki ambavyo ni Mahakama ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama ya Zanzibar na vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma ambavyo ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inashughulikia mambo yote ya Muungano kama yalivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Bara. Aidha, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inashughulikia mambo yote yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Zanzibar.
Sababu za kuwepo kwa Muungano
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umekuwepo kutokana na sababu mbalimbali kama vile:
Kuwepo kwa mahusiano ya karibu na ya kihistoria baina ya Tanganyika na Zanzibar katika nyanja mbalimbali kama vile udugu wa damu, biashara, utamaduni, lugha na mahusiano ya karibu kisiasa hususan baina ya vyama vya TANU na ASP.
Adhma ya kuwa na Muungano wa Afrika hususan kwa kuanzia na Shirikisho la Afrika Mashariki. Hata kabla ya uhuru wa Tanganyika, Mwalimu Nyerere pamoja na viongozi wengine waliokuwa wakipigania uhuru katika ukanda wa Afrika walikuwa na matarajio ya kuwa na Muungano wa Afrika. Mwalimu Nyerere binafsi alipendelea uwepo Muungano wa Afrika kwa kuanzia na Mashirikisho ya kikanda.
Kimsingi zipo sababu mbalimbali zilizosababisha Muungano huu kama vile historia za nchi hizi mbili, ukaribu wa nchi hizi mbili, muingiliano wa kijamii, ushirikiano wa kibiashara, ushirikiano madhubuti na wa muda mrefu wa kisiasa baina ya TANU na ASP, ushirikiano na urafiki wa muda mrefu kati ya watu, viongozi, na wakati wa harakati za utaifa uliopelekea uhuru wa nchi hizo mbili.
Hati ya Makubaliano ya Muungano
Msingi wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ni Hati za Muungano za mwaka 1964. Hati za Muungano zilitiwa saini na waasisi wa Muungano tarehe 22 Aprili, 1964 na kupelekea Tanganyika na Zanzibar kuwa dola moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Baada ya Muungano, Mwalimu J. K. Nyerere alikuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya ya Muungano wa Tanzania na Sheikh Abeid Amani Karume, alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aprili 26, 1964 Bunge la Tanganyika lilipitisha Sheria za Muungano. Halikadhalika, Sheria hizi zilithibitishwa na Baraza la Mapinduzi Zanzibar.
Sheria hizi za Muungano zilithibitisha Hati za Muungano, zilitaja Rais na Makamu wa Rais, zilitaja Muundo wa Muungano na Katiba ya Muungano. Aidha, Aprili 27, 1964 waasisi wa Muungano walibadilishana Hati za Muungano na wajumbe saba wa Baraza la Mapinduzi waliapishwa kuwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ni Sheikh Abeid Amani Karume, Kassim Abdala Hanga, Abdulrahaman Mohamed Babu, Hassan Nassor Moyo, Sheikh Aboud Jumbe, Hasnu Makame na Sheikh Idris Abdul Wakil. Baada ya kuapishwa kuwa Wabunge wakateuliwa kuwa Mawaziri wa Serikali ya Muungano.
Kabla ya Muungano, kulikuwa na Katiba ya Tanganyika ya mwaka 1962 na upande wa Zanzibar kulikuwa na Amri za Katiba (Decrees).Katiba ya Tanganyika baada ya kufanyiwa marekebisho ili kukidhi mahitaji ya Muungano iliendelea kutumika kama Katiba ya Muungano ya mpito hadi mwaka 1977 ilipopitishwa Katiba ya Muungano kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano na Sheria za Muungano.
Aidha, marekebisho hayo yalimtaja Rais wa Zanzibar kuwa ni Makamu wa Kwanza wa Rais, akiwa ni msaidizi wa Rais kwa masuala yote ya kiutawala kwa upande wa Zanzibar, na Waziri Mkuu kuwa ni Makamu 5 wa Pili wa Rais ambaye atamsaidia Rais kwa masuala yahusuyo upande wa Tanganyika na kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni.
Katiba ya muda ya mwaka 1965 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliainisha mambo kumi na moja ambayo yalikubalika kuwa ni ya Muungano chini ya usimamizi wa Serikali ya Muungano ambayo ni pamoja na Katiba na Serikali ya Muungano Mambo hayo ni: - Mambo ya Nchi za Nje, Ulinzi; Polisi ,Mamlaka juu ya mambo yanohusika na hali ya hatari, Uraia, Uhamiaji, Mikopo na Biashara ya Nchi za Nje na Utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Mambo mengine ni Kodi ya Mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa nchini Tanzania unaosimamiwa na Idara ya Forodha, na Bandari, mambo yanayohusika na usafiri wa anga, posta na simu.
Kuongezeka kwa mambo ya Muungano
Mambo ya Muungano yaliongezeka kutoka kumi na moja (11) hadi ishirini na mbili (22) kutokana na mahitaji ya ndani ya wananchi yaliyolenga kuunganika kwa mambo mengi zaidi pamoja na mabadiliko yaliyokuwa yanaendelea kutokea ulimwenguni baada ya Muungano.
Mwaka 1965 jambo la kumi na mbili linalohusu Mambo yote yanayohusika na sarafu na fedha kwa ajili ya malipo yoyote halali (pamoja na noti), mabenki (pamoja na mabenki ya kuweka akiba) na shughuli zote za mabenki, fedha za kigeni na usimamizi juu ya mambo yanayohusika na fedha za kigeni liliongezeka chini ya Katiba ya muda ya mwaka 1965.
Sababu kubwa ilikuwa ni kuwa na sarafu ya pamoja ya Tanzania baada ya Muungano, na kurahisisha usimamizi wa fedha za kigeni na mabenki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, kufuatia kuundwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1967, mambo matatu ya Muungano yaliongezwa, ambayo ni Leseni za viwanda na takwimu elimu ya juu, na usafiri na usafirishaji wa anga. Mwaka 1968, mambo ya maliasili ya mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa ya motokaa na ama ya petrol na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa na gesi asilia yaliongezwa kwenye orodha ya mambo ya Muungano. 13 Aidha mambo ya Muungano yaliendelea kuongezeka hadi kufikia 21 kufuatia kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977.
Mambo yote yaliyokuwa ya upande wa Tanganyika na Zanzibar yaliyokuwa yakisimamiwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki, yalikabidhiwa kwa Serikali ya Muungano. Mwaka 1992 kufuatia mabadiliko ya mfumo wa siasa nchini suala la ishirini na mbili la uandikishaji wa vyama vya siasa na mambo mengine yanayohusiana navyo liliongezwa kwenye orodha ya mambo ya Muungano.
HITIMISHO
Muungano umechukuwa nafasi kubwa katika kuwaunganisha wananchi na kuimarisha mahusiano mazuri baina ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka wigo mpana kwa wananchi wake kuweza kuzitumia fursa mbalimbali zilizopo za kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa lengo la kujipatia maendeleo. Ni vyema tukatumia ipasavyo fursa zilizopo Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kwa kuleta maendeleo yatakayoinua hali ya uchumi wa Watanzania. Ili tuweze kuzitumia vizuri fursa hizi hatuna budi tuulinde, tuuimarishe na kuudumisha Muungano wetu adhimu kwani ni dira ya maendeleo na mafanikio yetu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.