MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge amesema ili suala la lishe na afya ya mzazi na mtoto lipate mwitikio mzuri katika jamii ni lazima kushirikisha wadau na viongozi wa vijiji na mitaa kwani ndio wenye watu hadi ngazi ya kaya.
Dkt Mahenge ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa kikao cha mapitio ya viashiria vya huduma za afya ya uzazi na mtoto, pamoja na tathmini ya nusu mwaka ya utekelezaji wa viashiria vya mkataba wa lishe, amesema viongozi wa vijiji na mitaa ni watu muhimu kwa kuwa ndio wanaowajua watu vizuri.
“Hili swala ni muhimu sana ili lifanikiwe lazima tuwashirikishe wadau, na wadau wenyewe ni viongozi wa vijiji na mitaa hawa watatusaidia ndio wanaishi na hawa watu, wao ndio wanajua nyumba gani kuna mjamzito” amesema Dkt Mahenge.
Amesema katika juhudi zilizonyika na Serikali ya Mkoa imeanza kuleta matumaini lakini bado hawajafikia lengo lililotakiwa la kumaliza kabisa tatizo la lishe duni na huduma ya afya ya uzazi, huku kila kiongozi katika eneo lake kuhakikisha anakwenda kutoa elimu hiyo ili ifike vizuri ngazi ya jamii.
“Kwakweli tumejitahidi kwa kiasi flani lakini hatujafikia lengo, lengo ni kuona katika ripoti hatuna alama za njano au nyekundu na hili linawezekana kila mmoja kwenye eneo lake akitimiza wajibu wake” alisema.
Aidha amewakumbusha Wakurugenzi wa Halmashauri zote kuhakikisha wanatenga fedha kama walivyoagizwa lengo likiwa ni kuhakikisha zoezi hilo linafikia lengo katika kumaliza tatizo la huduma ya afya ya uzazi wa mama na mtoto na lishe bora ili kupunguza utapiamlo.
Amesema kukiwa na lishe bora katika jamii itakuwa ni kichocheo cha maendeleo katika nyanja za Afya, Elimu, Kilimo, Biashara na uchumi, hivyo pale tu ambapo athari za lishe duni au utapiamlo zitakapodhibitiwa au kutokomezwa malengo katika nyanja hizo yataweza kufikiwa kwa ufanisi.
Amesema kuwa lazima wote wafahamu kuwa wanawake wajawazito kuwa na lishe duni inawaweka katika mazingira hatarishi na kujifungua katika mazingira hatarishi, au kujifungua watoto njiti na pengine watoto wenye utindio wa ubongo au mimba kuharibika hivyo ni muhimu kuimarisha lishe katika jamii.
Akiwasilisha ripoti katika kikao hicho Mratibu wa Huduma za afya ya uzazi wa mtoto Mkoa wa Dodoma Nice Mosha, amesema wamekuwa wakiweka malengo mbalimbali na katika malengo hayo wamefanya shughuli mbalimbali katika kutekeleza mipango waliyojiwekea kupitia halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Dodoma.
Amesema katika malengo hayo wanatumia njia za uzazi wa mpango kwa malengo, na wamekuwa wakiwapa mafunzo mbalimbali watumishi katika kutekeleza elimu ya uzazi wa mpango, huku wakisisitiza kwa watoto wachanga lishe bora kwa siku 1,000 za mwanzo yani siku ya kwanza mimba kutungwa mpaka mtoto kufikisha umri wa miaka miwili.
“Wataalamu wanatuambia kuwa watoto waliopata huduma bora kilishe kipindi cha siku 1000 za mwanzo wa uhai wao wanapata faida zitakazo dumu katika maisha yao yote na pamoja na maendeleo mazuri ya ukuaji wa ubongo na uwezo mzuri wa kukabiliana na maradhi” amesema.
Amesema katika kutekeleza malengo ya kukuza au kuondoa matatizo ya afya ya uzazi na mtoto, sambamba na kuhimiza wataalamu wa afya kuhimiza wazazi kujifungulia katika hospitali na sio kujifungulia nyumbani ambako wanaweza kupata madhara mbalimbali.
Kuhusu tawimu za vifo vya uzazi na mtoto amesema vinaongezeka mwaka hado mwaka mbapo 2018 ilikuwa 67, 2019 ilikuwa 74, na 2020 ikawa 88, na mwenendo wa takwimu za vifo kwa watoto wachanga ni 2019 ilikuwa 694, na 2020 ikawa 681 ambapo ilishuka kidogo.
Kwa upande wake Afisa lishe wa Mkoa wa Dodoma Herieth Carin amesema Oktoba 18, 2018 walisaini mkataba wa hafua za lishe na wamekuwa wakitekeleza kupitia halmashauri na wao wamesaini mikataba hiyo hadi ngazi za chini kuhakikisha wanatimiza malengo ya hafua za lishe kuondoa tatizo la lishe katika jamii.
Amesema wamekuwa wakitenga fedha na halmashauri zimekuwa zikitenga fedha ili kutekeleza maswala mbalimbali ya lishe na kila Halmashauri zimekuwa zikitakiwa kutenga shilingi elfu moja kwa kila mtoto katika maswala ya lishe.
Kwa mwaka unaoendelea kutekelezwa walipanga kutenga zaidi ya shilingi milioni mia tano ishirini na tisa, (529) na hadi nusu ya m waka walitenga zaidi milioni 223 na mpaka sasa fedha zilizotolewa ni shilingi milioni 136 sawa na asilimia 61 ya fedha hizo.
Nae Mkurugenzi wa kitengo cha afya ya uzazi na mtoto kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Bi Jackline Ndanshau, akizungumza katika kikao amewataka wataalamu wa afya katika hospitali kuacha kukaa na wagonjwa ambao hawana uwezo nao hilo ndio hupelekea kupata vifo vya uzazi.
“Unakuta unaenda kwenye kituo cha afya una mkuta mgonjwa kachoka na hawezi kuhudumikwa pale na wewe ukifika ndio unatoa rufaa aende hospital kubwa na mda mwingine tunakuwa tumechelewa, na kwanini ukae na mgonjwa ambae huna uwezo nae? Toa fufaa” amesema.
Aidha ametaka kurudishwa kwa utaratibu wa kufanya posimotam kila asubuhi kujua utendaji wa kazi hasa katika vifo vya mama na mtoto ili kujua chanzo na namna ya kutatua changamoto hizo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.