WANANCHI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na viunga vyake wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika wiki ya maadhimisho ya kitaifa ya kupinga magonjwa yasiyoambukiza na kushiriki michezo mbalimbali katika uwanja wa michezo wa Jamhuri jijini hapa.
Kauli hiyo imetolewa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Dkt. Gatete Mahava alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake leo.
Dkt. Mahava alisema kuwa maadhimisho ya wiki ya kupinga magonjwa yasiyo ya kuambukiza itaanza tarehe 9-14 Novemba, 2019 katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Napenda kutumia nafasi hii kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika uwanja wa michezo wa Jamhuri na kushiriki katika michezo mbalimbali itakayokuwa ikichezwa katika uwanja huo” alisema Dkt Mahava. Aidha, aliitaja michezo itakayochezwa katika maadhimisho hayo kuwa ni mpira wa miguu, mpira wa kikapu, riadha, kuvuta kamba na netiboli. Michezo hiyo itakuwa ikichezwa kila siku, aliongeza.
Akiongelea magonjwa yasiyoamkubiza, alisema kuwa magonjwa hayo, yanatokana na mfumo wa maisha ya mwanadamu unaomfanya kutoushughulisha mwili. Mfumo huo unasababisha mwili kukosa mazoezi na hatimae kupelekea magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari, shinikizo la damu, moyo, kiharusi, saratani, pumu, sikoseli, afy ya akili, macho, kinywa na meno na ajali. Uzinduzi huu utajumuisha shughuli mbalimbali kama vile tamasha la michezo, kongamano la kisayansi, maonesho, huduma za uchunguzi wa afya na elimu ya afya.
Maadhimisho hayo yataongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Tutembee pamoja katika kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza’.
Maadhimisho hayo yanayofanyika katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma yanaratibiwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.