Na. Hellen M. Minja
Habari – DODOMA RS
Wito umetolewa kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma kubadilika kwa kufuata Sheria za nchi kwani pasi na hivyo, watafichuliwa kupitia Mfumo wa kisasa wa Kamera za barabarani na mitaani (CCTV) zilizofungwa kwenye maeneo kadhaa ya Jiji la Dodoma wakifanya matendo ya kihalifu na watachukuliwa hatua za kisheria.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameyasema hayo Septemba 30, 2025 alipokua kwenye ziara ya ukaguzi wa Mradi wa kusimika Kamera za barabarani kwenye maungio ya barabara za kuingia na kutoka Mkoa wa Dodoma kwa lengo la kuimarisha ulinzi ndani ya Jijini hili la Makao Makuu ya nchi.
“Nitoe wito kwa wananchi wa Dodoma wabadilike kwa kufuata sheria na taratibu za nchi kwani wasipofanya hivyo wataonekana kupitia Mfumo wa Kamera za barabarani wakifanya uhalifu na watakapoonekana wakitenda kinyume cha taratibu, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao”.
Aidha, Mhe. Senyamule ameongeza kuwa kupitia Teknolojia hiyo ambayo Kamera zitawekwa kwenye maeneo makubwa, italeta sifa kwa wageni kuingia na kuwekeza kutokana na uhakika wa usalama hivyo amewaasa wananchi kuilinda miundombinu ya Serikali kwani imewekwa kwa faida yao.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri amesema zoezi hilo lililogharimu kiasi cha shilingi Milioni 473, linaunga mkono juhudi za ujio wa Serikali Mkoa wa Dodoma pamoja na kutimiza ndoto ya Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuifanya Dodoma kuwa sehemu salama kwa uwekezaji na utalii.
Vile vile, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Wislance Smart System Bw. Wisley A. Ussiri ambao wanatekeleza Mradi huo amesema Mradi huo umelenga njia kuu nne za kuingia na kutoka Jiji la Dodoma ambapo utekelezaji wake umefikia 90% na Kamera zilizofungwa ni za kisasa zenye kuleta tija kwani zinaonesha picha zenye ubora wa hali ya juu.
Mradi wa kusimika Kamera za barabarani katika Mkoa wa Dodoma umetumia siku 90 sawa na Miezi mitatu ya utekelezaji ambapo nguzo 50 zilizobeba jumla ya Kamera 106 zenye uwezo wa kutumia teknolojia ya kisasa ya Akili Mnemba zimesimikwa.
 
                              
                              
                            1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.