Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WILAYA ya Dodoma ilizalisha tani 48,413 za mazao ya chakula na biashara katika msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023 ukiifanya hali ya chakula kuwa ya wastani.
Taarifa hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Wilaya ya Dodoma, Sakina Mbugi alipokuwa akisoma risala ya utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru Wilaya ya Dodoma kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Chamwino jijini Dodoma.
Mbugi alisema “Mheshimiwa Rais; hali ya chakula kwa sasa ni ya wastani kutokana na mavuno yaliyopatikana msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023. Wilaya ilizalisha tani 48,413 za mazao ya chakula na biashara. Katika msimu wa kilimo wa 2022/2023 eneo lililolimwa kwa ajili ya mazao ya chakula ni hekta 18,522 ambazo zilizalisha tani 23,682 za mavuno. Kwa mazao ya biashara eneo lililolimwa ni hekta 20,869 na zilizalisha tani 24,731. Bei za vyakula sokoni ni za wastani. Shilingi 18,653,976 zimetumika kutekeleza miradi ya ukarabati wa Bwawa la Umwagiliaji Ipala na shamba la mafunzo la Msalato”.
Akiongelea sekta ya mifugo alisema kuwa wilaya ilitoa shilingi 26,927,000 kwa ajili ya zoezi la chanjo ya homa ya mapafu kwa ng’ombe na mbuzi. “Ng’ombe 41,258 na mbuzi 9,370 walichanjwa. Shilingi 9,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa “shade“ za mizani mbili ya ng’ombe zilizotolewa na serikali katika mnada wa Hombolo na Msalato. Serikali ilitoa ruzuku ya dawa lita 96 za kuogeshea mifugo, shilingi 5,008,000 kwa ajili ya ujenzi wa birika la kunyweshea mifugo katika Kata ya Ipala. Wilaya ilitoa shilingi 16,670,650.00 kwa ajili ya ujenzi wa makaro mawili na shilingi 15,800,000 kwa ajili ujenzi wa uzio wa mifugo“ alisema Mbugi.
Kuhusu sekta ya uvuvi alisema kuwa wananchi walihamasishwa kuanzisha mabwawa 123 ya samaki kwa ajili ya kuboresha kipato na lishe. “Shirika la Save the Children lilitoa msaada wa vifaranga vya samaki aina ya Sato kwa wafugaji wanne na kikundi kimoja katika Kata za Msalato, Miyuji, na Hombolo Makulu. Vifaranga 6,000 vilipandwa na chakula cha Kg 150 kilitolewa” alisema Mbugi.
Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 unaongozwa na kaulimbiu isemayo “Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa ustawi wa Viumbe Hai kwa Uchumi wa Taifa”
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.