HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imebuni vyanzo mbadala vya mapato nje ya viwanja katika kuhakikisha inapunguza utegemezi wa mapato ya viwanja na inakua na mapato endelevu wakati wote.
Mkurugenzi wa Jiji, Godwin Kunambi ameema halmashauri hiyo imepunguza upimaji wa viwanja katika mwaka 2019/20 kwa asilimia tano lakini bado bajeti ya mapato ya ndani imeongezeka kwa asilimia 8.7.
Amesema mbali na kupungua kwa mapato yanayotokana na viwanja, mwaka 2018/19 viwanja vilivyokasimiwa vilikuwa 20,000 ambavyo bajeti yake ilikuwa Sh bilioni 59.1 sawa na asilimia 37 ya bajeti yote ya mwaka huo ambayo ni sh bilioni 159.5.
Alisema katika mwaka wa fedha 2019/20, viwanja vinavyokadiriwa kupimwa ni 10,000 sawa na mapato ya Sh bilioni 49 ambavyo ni sawa na asilimia 27 ya bajeti yote kwa mwaka huo wa fedha ambayo ni Sh bilioni 161.9.
“Katika bajeti hii, Sh takribani bilioni 24 ni mapato kutoka kwenye vyanzo vingine vya ndani. Kwa hiyo pamoja na kupungua kwa upimaji wa viwanja kwa asilimia tano bado bajeti ya mapato ya ndani imeongezeka kwa asilimia 8.7,” amesema.
Kunambi amesema vyanzo vinavyoongezeka licha ya viwanja ni pamoja na ushuru wa huduma Sh bilioni 1.0, idara ya usafi wa mazingira Sh bilioni 1.4, leseni za biashara sh bilioni 1.1 na mapato kutoka kitengo cha matofali Sh bilioni 1.0.
“Vyanzo vingine vinavyochangia fedha katika makusanyo nje ya viwanja ni maeneo ya uwekezaji ambavyo kwa sasa ni Sh bilioni 10. Lakini, vitaanza kuingiza fedha baada ya kukamilika kuanzia nusu ya pili ya mwaka 2019/20,” alisema.
Chanzo: Tovuti ya HabariLeo
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.