IDARA ya Elimu Sekondari katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma imetoa tuzo kwa Afisa Elimu na Vifaa Fredrick Mwakisambwe kwa kutambua mchango wake katika kusimamia kazi za kila siku za utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa madarasa 147 katika Halmashauri hiyo kupitia program ya Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 ambayo yamekamilika hivi karibuni.
Tuzo hiyo imekabidhiwa kwa mtumishi huyo na Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari wa Jiji la Dodoma Upendo Rweyemamu wakati wa kikao cha wadau wa elimu jijini humo kilichofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari ya Dodoma leo Januari 5, 2022.
Akizungumza wakati wa kukabidhi tuzo hiyo, Rweyemamu alisema yeye kama Mkuu wa Idara na wasaidizi wake wameamua kumpatia Mwakisambwe zawadi hiyo kwa kujitoa kwake usiku na mchana katika kufuatilia na kuratibu kazi za ujenzi wa madarasa hayo kila hatua akisadiana na wakuu wa shule na kamati zao za ujenzi.
Alisema anaamini tuzo hiyo itamuongezea moyo na ujasiri wa kufanya kazi kwa bidii zaidi katika majukumu yake ya kila siku na kwamba itakuwa ni kumbukumbu katika maisha yake kwa kushiriki kwa mafanikio katika mradi huo wa madarasa ambao ni wa kitaifa ambao umetekelezwa nchi nzima.
Kwa upande wake Afisa Elimu Mwakisambwe alimshukuru Mkuu huyo wa Idara kwa niaba ya watumishi wengine wote wa Idara, Wakuu wa Shule, pamoja na wadau wengine alioshirikiana nao katika kusimamia mradi huo.
Alisema tuzo hiyo ni heshima kubwa kwake na itamuongeza nguvu zaidi na ari ya kufanya kazi kwa bidii.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.