Na. Theresia Nkwanga, Dodoma
AFISA Elimu Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Upendo Rweyemamu amesema mashindano ya Mdahalo kwa shule za Sekondari yafanyike kwenye ngazi ya shule ili kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujiamini , kuzungumza , kujielezea na kuandika kwa lugha ya Kiingereza.
Hayo aliyasema alipohudhuria fainali za Mashindano ya Mdahalo kwa shule za Sekondari Dodoma yaliyofanyika tarehe 10 Oktoba,2022 katika ukumbi wa Dodoma Sekondari.
Rweyemamu alisema kumekuwa na mashindano ya mdahalo kwa shule za Halmashauri ya Jiji la Dodoma ngazi ya Wilaya ni wakati sasa mashindano yafanyike kwenye ngazi ya shule kati ya darasa na darasa ili kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuzungumza na kuandika kwa lugha ya Kiingereza.
Akiongelea umuhimu wa midahalo katika taaluma Rweyemamu alisema midahalo inamjengea mwanafunzi ujasiri wa kujielezea , kujenga hoja, inamuongezea misamiati ya lugha ya kiingereza, inamjengea ujasiri pia inaongeza ufaulu kwa wanafunzi.
“Tunaenda kuongeza ufaulu katika shule zetu sababu wanafunzi wanaenda kuwa vizuri kwenye lugha ya kiingereza, mwanafunzi anaweza akawa ameelewa swali lakini hana misamiati yakutosha ataishia kujua kichwani mwake lakini atashindwa kuweka kwenye maandishi kupitia midahalo mwanafunzi ataongeza misamiati na kumudu masomo yake pamoja na mitihani anayoulizwa kwa lugha ya kiingereza”, alisema Rweyemamu
Kwa upande mwingine, Mratibu wa shindano la Mdahalo kwa shule za Sekondari Dodoma, Malick Masoud alisema lengo la mashindano haya nikuwajengea wanafunzi uwezo wa kujiamini, kuwakuza kitaaluma, kuchangamsha ubongo wao kupitia mada mbalimbali zinazojadiliwa pia kuwakutanisha pamoja kama wanafunzi wa Dodoma .
Aliongezea kwa kuzipongeza shule zote zilizoshiriki mashindano ya Mdahalo kwa shule za Sekondari Dodoma na kuzitia moyo shule ambazo zilitoka mapema kwenye mashindano kutokukata tamaa pia alitoa chachu kwa shule ambazo hazijashiriki kujiandaa kwa awamu ijayo ya mashindano.
“Tumepokea simu nyingi kutoka kwa baadhi ya shule wakiuliza kwa nini sisi hatujashiriki, napenda kuwaambia huu ni mwanzo tu awamu inayofuata shule zote za Halmashauri ya Jiji la Dodoma zitashiriki”.
Naye Nadhifa Ayubu, mwanafunzi kutoka Viwandani Sekondari alimshukuru Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri kwa kuanzisha shindano hili kwani linawajengea uwezo wa kujieleza mbele za watu hivyo, kuwafanya wajiamini pia kuelewa lugha ya kiingereza ambayo inatumika kujifunzia kwa elimu ya Sekondari.
Mashindano ya Mdahalo kwa shule za Sekondari Dodoma yalianza tarehe 01 Oktoba, 2022 yakihusisha shule ya Mkonze, Mnadani, Miyuji ,Kisasa, Dodoma Sekondari, Viwandani, Sechelela, Nzughuni, Kikuyu, Hazina, Nghong’onha na Kiwanja cha Ndege na yalihitimishwa tarehe 10 Oktoba, 2022 huku shule ya Sekondari Miyuji ikiibuka mshindi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.