AFISA Elimu Msingi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Joseph Mabeyo anaridhishwa na muitikio chanya wa wanafunzi katika vipindi vya masomo vinavyoendelea katika redio mbalimbali za Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Kauli hiyo ameitoa katika kipindi cha mahojiano cha ‘Dodoma Live’ kinachorushwa na kituo cha redio cha Dodoma FM leo.
Mwalimu Joseph Mabeyo amesema kuwa tangu kuanza kwa program ya kuwafundisha wanafunzi kupitia redio, idadi ya wanafunzi wanaozurura mitaani imepungua sana katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Shukrani kwa menejimenti ya redio Dodoma FM kwa kukubali kurusha vipindi vya elimu katika redio yenu, jambo hili ni ukombozi kwa kizazi hiki. Mabadiliko makubwa yanaonekana kwa wanafunzi na uzururaji umepungua na wanafunzi wanasoma kwelikweli. Hii pia inaonesha kuwa wanafunzi na wazazi wameelewa dhamira ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma” amesema Mwalimu Mabeyo.
Akiongelea program hiyo, Afisa huyo amesema kuwa program hiyo ilianza kwa kuwabaini walimu wabobezi na mahili katika masomo yote yanayofundishwa. “Walimu hao waliandaa masomo ya kufundisha kwa kufuata taratibu za uandaaji wa masomo kwa kuanza na andalio. Na kila somo lililoandaliwa lilihaririwa ili kujiridhisha na ubora na usahihi kabla ya kurushwa katika redio” amesema Mwalimu Mabeyo.
Akijibu swali la mwananchi aliyepiga simu kutaka kujua kuwa kama program hiyo imeziacha nje shule za binafsi, Afisa Elimu Msingi amesema kuwa shule hizo hazijaachwa. “Shule za binafsi hazijaachwa. Shule hizo zilikuwa na utaratibu wake wa kutoa ‘home package’ kwa wanafunzi wao. Tunaenda Pamoja, mfano somo la Kiingereza na somo la Kiswahili yanafundishwa sawa kwa shule za binafsi na za serikali” amesema Mwalimu Mabeyo.
Ikumbukwe kuwa mkakati wa kuwanusuru wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wa Jiji la Dodoma ulizinduliwa na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi tarehe 28 Aprili, 2020 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.