Na Nemes Michael, DODOMA
AFISA Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu amesema kuwa ushindi katika michezo hutengenezwa kwa umoja, mshikamano, utayari na muelekeo chanya kwa kila mshiriki pamoja na kudumisha nidhamu.
Mwalimu Rweyemamu ameyasema hayo leo katika viwanja vya Shule ya Sekondari Dodoma wakati wa hitimisho la michezo ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) ngazi ya Mkoa Jijini hapa, ulioenda sambamba na kaulimbiu isemayo "Michezo, sanaa na taaluma kwa maendeleo ya uchumi wa viwanda."
“Sasa tunamaliza mashindano na kuvunja timu zetu zilizokuwa katika mashindano kwa kutengeneza timu moja ya watoto 100 waliotoka katika Halmashauri zote nane, Naamini kwa jinsi tulivyojiandaa ushindi lazima tuupate” aliongeza Mwalimu Rweyemamu.
Naye, Afisa Michezo na Utamaduni wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Peter Ititi amesema kwa mwaka 2021 michezo ya ngazi ya sekondari UMISSETA imekuwa tofauti na miaka iliyopita na amewapongeza watoto wa kike kwa kuleta ushindani na kuamua kushiriki katika mashindano hayo kwa kiwango kubwa.
“Kumekuwa na hamasa kubwa kwa mwaka huu, watoto wanaonesha kiasi gani wameelewa kuwa michezo ina maana gani kwa upande wao, nidhamu waliyonayo ni nzuri pia ni njia sahihi katika kufika wanapotaka lakini juhudi zinahitajika katika yote” alisema Ititi.
Kwa upande wake, Gervas Fred Mwanafunzi wa Shule ya sekondari St. Peter Clever amabaye ni kapteni wa mpira wa kikapu Halmashauri ya Jiji la Dodoma amesema kuwa mafanikio waliyoyapata kwa kuchukua vikombe 9 kati ya 12 vilivyokuwemo ni juhudu za ushirikiano kuanzia waalimu mpaka kufikia kwao kwa kuamua kufanya maamuzi sahihi kwa pamoja.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.