WANAFUNZI wote wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kufuatilia vipindi vinavyoendelea katika redio zilizopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili waweze kuendelea na program ya masomo wawapo nyumbani.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu alipokuwa akiongea katika kipindi cha ‘Dodoma Live’ kinachorushwa na kituo cha redio cha Dodoma FM jana asubuhi.
Mwalimu Rweyemamu amesema kuwa program ya kuwafundisha wanafunzi kupitia redio inalenga kuwafundisha wanafunzi walio katika madarasa ya mitihani. Madarasa hayo ni darasa la nne na darasa la saba kwa shule za msingi na wanafunzi wa kidato cha pili na nne kwa sekondari, amesema. Utaratibu huu ni mwanzo wa program hii, “mpango wetu ni kufundisha madarasa yote katika kipindi kijacho. Masomo haya tunayofundisha wanafunzi wote wanatakiwa kuyafuatilia. Mfano, tunapofundisha kidato cha pili, wanafunzi wa kidato cha tatu na cha nne wanaweza kufuatilia na kujifunza kama marejeo ya kile walichojifunza. Wanafunzi wa shule ya msingi vivyo hivyo” amesema Mwalimu Rweyemamu.
Akiongelea ratiba ya vipindi vya redio, amesema kuwa ratiba hiyo imeandaliwa kwa vipindi na redio zote katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Ratiba inapatikana katika tovuti ya Jiji, www.dodomacc.go.tz pamoja na “home packages zipo kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi kufanya mazoezi zaidi”. Ratiba hiyo pia inapatikana kwa walimu wakuu, wakuu wa shule na kwa maafisa elimu kata wote wa jiji la Dodoma. Aidha, tumewaandikia barua viongozi wa dini na kuwatumia nakala za ratiba hiyo ili wasaidie kuwafikishia waumini wao” amesema Mwalimu Rweyemamu.
Ikumbukwe kuwa mkakati wa kuwanusuru wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wa Jiji la Dodoma ulizinduliwa na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi tarehe 28 Aprili, 2020 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Afisa Elimu ya Msingi wa Jiji la Dodoma Mwalimu Joseph Mabeyo (kushoto) na Afisa Elimu ya Sekondari Mwalimu Upendo Rweyemamu (katikati) walipokuwa wakishiriki kipindi cha mahojiano cha 'Dodoma Live' katika redio ya Dodoma FM jana na kuelezea juu ya utekelezaji wa mkakati kufundisha wanafunzi walio nyumbani wakati wa kipindi hiki ambacho shule zimefungwa ili kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona. Kulia ni mtangazaji wa redio ya Dodoma FM.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.