SERIKALI imesema itaendelea kuwekeza kwenye maeneo tofauti yanayohusu afya ya kinywa na meno na tasnia zinazoambatana na kada hiyo ili kuboresha afya ya Kinywa na Meno nchini.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa leo tarehe 21 Novemba, 2022 Jijini Mwanza katika Ukumbi wa TFDA na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya Prof. Paschal Rugaje wakati akifungua kikao kazi cha Waganga Wakuu wa Mikoa wa Afya ya Kinywa na Meno na baadhi ya Wataalam hao kutoka kwenye baadhi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Akimwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumani Nagu, Prof. Paschal Rugaje amesema takwimu zinaonyesha kuwa watanzania wengi wanakabiliwa na matatizo makubwa yanayotokana na afya ya kinywa na meno kote nchini na ndiyo maana imeamua kuwekeza katika eneo hilo.
“Serikali imeendelea kuwekeza katika nafasi za mafunzo ya madaktari wa magonjwa ya afya ya kinywa na meno, pia tasnia nyingine ambazo zinaambatana na madaktari wasaidizi, wauguzi, mafundi wa mitambo kwa ajili ya meno (Biomedical Engineers), vifaa tiba vya meno na pia katika kuajiri watumishi” amesema Prof. Rugaje.
Aidha, amesema afya ya kinywa na meno ni muhimu sana na ni tatizo, kwani takwimu zinaonyesha kuwa katika kila watu wazima wanne, watatu wameoza meno, katika kila watoto watatu, mmoja ameoza meno na katika kila watu kumi mmoja anatatizo la fizi.
Prof. Rugaje pia amesema kuwa kwa hali ilivyo sasa ni hospitali za Mikoa na za juu yake ndizo zinazotoa huduma ya afya na kinywa kwa uhakika lakini matarajio na mipango ya Serikali ni kuhakikisha kuwa vituo vya afya na hospitali za Halmashauri ziwe zinatoa huduma hiyo ifikapo mwaka 2025.
Kwa upande wake Dkt. James Kengia akiongea kwa niaba ya mkurugenzi wa Idara ya Afya na Ustawi wa Jamii Ofisi ya Rais TAMISEMI amesema kwa hivi sasa Hospitali 142 za Halmashauri zinatoa huduma ya afya ya kinywa na meno.
Naye Dkt. Baraka Nzobo Kaimu Mkurugenzi anayeshughulikia huduma ya Afya ya Kinywa na Meno Wizara ya Afya amesema Wizara ya Afya itaendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo mbalimbali vya habari pamoja na msisitizo wa elimu mashuleni ili kupata jamii yenye afya ya kinywa na meno.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wajumbe, Dkt. Mohamed Mpunjo Mganga Mkuu wa Kinywa na Meno Mkoa wa Lindi amesema maelekezo yote ya Serikali yaliyotolewa ikiwa ni pamoja na machapisho, huduma, kubuni na kuandika maandiko ya miradi watayatekeleza kwa wakati.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.