AHADI ya Rais John Magufuli ya kuifungua Wilaya ya Mpwapwa kwa miundombinu imetimia katika muda mfupi kwa kuanza ujenzi wa barabara za lami na hivyo wilaya hiyo itaunganishwa na barabara kuu za Dodoma-Iringa na Dodoma-Morogoro hivi karibuni.
Rais Magufuli alitembelea wilaya hiyo mwaka jana na kuahidi kutoa fedha kujenga miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami Mpwapwa ambayo ni wilaya kongwe lakini ina kipande cha kilometa moja tu ya barabara ya lami mjini hapo.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Jabir Shekimweri akizungumza wakati wa ziara ya siku mbili ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyopewa fedha na serikali, alisema ahadi ya Rais imeanza kutekelezwa katika muda mfupi na wilaya hiyo imekuwa na barabara za lami.
Shekimweri alimpongeza Rais John Magufuli kwa ahadi aliyotoa ya kujenga barabara za lami kilometa tano mjini hapo, ambapo tayari Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) imeshajenga kilometa tatu kati ya tano.
Shekimweri alisema pia barabara ya Mpwapwa - Kongwa itajengwa kilometa 30 kutokana na ahadi iliyopo ndani ya Ilani ya Uchaguzi ya 2020-2025, hivyo barabara hiyo itajengwa kilometa 35 na itabakia kidogo kuunganishwa na lami wilayani Kongwa.
Pia wilaya hiyo itafunguka kwa barabara ya lami kutoka Mpwapwa-Kibakwe yenye urefu wa kilometa 75 mara baada ya upembuzi yakinifu pamoja na ya mchepuko kuingia Kituo cha Mwendokasi Ving’awe hapo Godegode na hatimaye kuunganishwa na barabara ya Iringa-Dodoma.
Akielezea ujenzi huo, Meneja wa TARURA Wilaya ya Mpwapwa, Emmanuel Lukumay alisema tayari kilometa tatu kati ya kilometa za ahadi ya Rais Magufuli kujenga barabara za mjini zimeshakamilika na zilizobaki ujenzi unaendelea.
Naye Meneja wa Tanroads Wilaya ya Mpwapwa, Salome Kabunda alisema tayari wameshajenga kilometa mbili kati ya tano ambazo wanatakiwa kujenga katika barabara itokayo Mpwapwa kwenda Kongwa ambayo itagharimu Sh bilioni 4.9.
Kabunda alisema gharama hizo ni kubwa kutokana na ukweli kwamba barabara hiyo ambayo ilikuwa ikikumbwa na mafuriko mara kwa mara, itainuliwa tuta juu mita tatu, itajengwa madaraja makubwa sita na mengine madogo.
Dkt. Mahenge baada ya kukagua barabara za mjini, kwanza alipongeza juhudi zilizofanywa na Tarura kwa gharama ya Sh milioni 907 kwa ajili ya kujenga barabara za mjini ambayo ni ahadi ya Rais Magufuli na imetekelezwa ndani ya muda mfupi kwa vitendo.
Kuhusu daraja la Miembeni lililosombwa na mafuriko, Lukumay alisema tayari wanatafiti aina ya udongo wa eneo hilo kwa kutumia watalaamu wa Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) hivyo wanachunguza ili kujipanga kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa gharama ya sh milioni 500.
Kwa upande wa Tanroads, Dkt. Mahenge aliwapongeza kwa kuanza ujenzi wa barabara ya Mpwapwa-Kongwa kwa kiwango cha lami ambayo ilikuwa mara kwa mara inakatika kwa mafuriko ya maji.
Dkt. Mahenge alimpongeza Rais Magufuli kwamba amekuwa akiahidi na kutekeleza ahadi zake katika kipindi kifupi, ametoa fedha na sasa barabara hizo zinajengwa kwa kiwango cha lami na kuunganisha wilaya hiyo na barabara kubwa za Dodoma-Morogoro na Iringa-Dodoma kwa kiwango cha lami.
Wilaya ya Mpwapwa ndiyo Kongwe pamoja na Kondoa, lakini ndiyo wilaya pekee ambayo ilikuwa haijaunganishwa na barabara za lami, lakini katika awamu ya tano wilaya hiyo itafunguka kwa kuwa na lami na kuuganishwa na barabara kuu kupitia Kongwa na Jimbo la Kibakwe barabara kuu ya Iringa-Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge (wa pili kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Jabir Shekimweri (wa kwanza kulia) wakimsikiliza Mhandisi (wa kwanza kushoto) akisoma taarifa maendeleo ya kazi ya ujenzi wa barabara Mpwapwa.
Picha za matukio ya ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge alipotembelea Wilaya ya Mpwapwa kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.