MKURUGENZI wa Idara ya Habari – Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa ameongea na waandishi wa habari kuhusu maelekezo yaliyotolewa kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri kufuatia ajali ya ndege ya Kampuni ya Precision Air kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO jijini Dodoma.
Kikao hicho kimefanyika leo tarehe 14, 2022 jijini Dodoma nakupokea taarifa ya awali ya ajali ya ndege ya Kampuni ya Precision Air iliyotokea mnamo Novemba 6, 2022 wakati wa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba na hatua zilizochukuliwa baada ya ajali.
Ajali hii ilihusisha ndege aina ya ATR 42-500 yenye namba PW 494 iliyokuwa ikisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza kupitia Bukoba ikiwa na watu 43 ambapo 39 walikuwa ni abiria na 4 walikuwa ni wafanyakazi wa ndege yaani Rubani na msaidizi wake na Maafisa Usalama ndani ya ndege 2 (Air Hostess). Ajali hii ilisababisha vifo vya watu 19 na majeruhi 26 ambao wote wametibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Baraza la Mawaziri limewaelekeza Wataalam wa ndani kushirikiana na Wataalam kutoka nje ya nchi katika kufanya uchunguzi kuhusiana na ajali hii ili kupata chanzo cha ajali na kutoa mapendekezo ya hatua zinazotakiwa kuchulikuliwa mara baada ya ajali kutokea.
Maelekezo ya Baraza yametolewa kwa kuzingatia kwamba nchi yetu imesaini mikataba mbalimbali ya Kimataifa ambayo inasimamia usafiri wa anga na hatua zinazopaswa kuchukuliwa mara baada ya ajali ya anga kutokea.
Vilevile, Baraza hilo limeelekeza vitengo vyote vinavyohusika na kukabiliana na majanga viimarishwe kwa namna mbalimbali ambazo zitatuwezesha sisi kama nchi kuongeza uwezo zaidi ya tulioano sasa katika kukabililana na majanga pale yanapotokea.
Kwa mujibu wa taratibu za kukabiliana na ajali za ndege, timu ya uchunguzi wa ajali na matukio ya ndege inapaswa kutoa taarifa ya awali (Accident Bulletin) ndani ya siku 14. Itafuatiwa na taarifa ya awali (Preliminary Report) itakayotolewa ndani ya siku 30 na hatimaye taarifa kamili (Final Report) itakayotolewa ndani ya miezi 12 baada ya ajali kutokea.
Aidha, Serikali inawaomba wananchi wote kuendelea kuwa watulivu wakati uchunguzi huu unafanyika na baada ya uchunguzi kukamilika wananchi watajulishwa. Pia,Baraza linawashukuru na kuwapongeza wananchi na wote waliohusika katika uokozi baada ya ajali hii kutokea.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.