Serikali imesema itatoa ajira mpya 12,000 za walimu wa shule za msingi na sekondari baada ya utaratibu wa kuajiri kukamilika kwa lengo la kuboresha sekta ya elimu nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo alipokuwa akitoa mrejesho wa mafanikio kwa wananchi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya sekta ya elimu yaliyotekelezwa ndani ya miaka mitano ya serikali ya awamu ya tano katika siku maalum ya TAMISEMI (TAMISEMI DAY -Elimu) jijini Dodoma.
Waziri Jafo amesema kuwa zaidi ya walimu 18,000 wameajiriwa na kupelekwa Shule za Msingi na Sekondari na ajira mpya 12,000 ziko katika taratibu za mwisho kuweza kukamilika kutokana na maelekezo yake Rais, Dkt. John Pombe Magufuli.
Amesema “changamoto ni nyingi na haziwezi kuisha ila Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameelekeza kuongeza ajira za walimu hivyo taratibu zikikamilika watanzania wapate kuchangamkia fursa hiyo”.
Aidha, Waziri huyo amesema kuwa mafanikio yaliyopatikana kwa miaka mitano katika Sekta ya Elimu ya Msingi na Sekondari ndani ya kipindi cha muda mfupi, kiasi cha Shilingi Trilioni 1.09 zimetumika kutoa elimu bila malipo kwa watanzania.
“Zaidi ya Shilingi Bilioni 502 zimetolewa kwa ajili ya elimu ya Msingi na Shilingi Bilioni 593.9 zimetumika katika shule za sekondari, jambo ambalo limesaidia watoto wa watanzania wenye kipato cha chini kupata elimu” ameeleza Waziri Jafo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mhandisi Joseph Nyamhanga, amesema uwekezaji na maboresho yaliyofanyika katika sekta ya elimu kwa shule za msingi na sekondari umesaidia kuongeza kiwango cha ufaulu katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa asilimia 81.50 mwaka 2019.
Naibu Katibu Mkuu, TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, Gerald Mweli, amesema Mpango wa elimu bila malipo ulianzishwa baada ya kufanyika utafiti na kugundua idadi kubwa ya watoto wakitanzania walikuwa hawaendi shule kutokana na wazazi na walezi kukosa ada.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.