MBUNGE wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde ametoa rai kwa wakina mama wa Jiji la Dodoma kuchangamkia fursa za kiuchumi ili kujiimarisha zaidi kiuchumi na kukuza kipato chao.
Mavunde ameyasema hayo jana wakati akitoa salamu katika kongamano la wakinamama linalojulikana kama Dodoma Capital City Gala lililofanyika katika ukumbi wa Mabele Jijini Dodoma.
“Kufuatia uamuzi wa Serikali kuhamishia shughuli zake hapa Dodoma, kumejitokeza fursa nyingi za kiuchumi na mahitaji makubwa ya huduma za kijamii.
Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa Jijini Dodoma, uwekezaji ambao ni kichocheo cha kukuza uchumi hapa Dodoma. Miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara, majengo na uwanja wa ndege inatekelezwa hapa na inatoa fursa za kutosha za kiuchumi, hivyo niwaombe wakina mama msikae nyuma muwe mstari wa mbele kuzikimbilia na kukamata fursa hizi.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekuwa ikitoa mikopo kwa makundi maalum wakiwemo wanawake ambapo mpaka sasa tangu mwaka 2015 zimetolewa jumla ya shilingi Bilioni 9 kama mkopo wa asilimia 10 ya mapato ya ndani, hivyo ni vyema kuitumia fursa hii kujipatia mitaji ya kuendesha shughuli zenu za kiuchumi” Alisema Mavunde.
Hafla hiyo iliyohudhuriwa na wanawake zaidi ya 500 wa Jiji la Dodoma ilihusisha pia maonesho ya bidhaa za wajasiriamali za wakina mama pamoja na semina iliyotolewa na wazungumzaji mbalimbali kwa lengo la kuwajengea uwezo na maarifa wakina mama.
Mgeni Rasmi katika hafla hiyo alikuwa ni Mh. Shally Raymond ambaye ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Wabunge Wanawake aliyeambatana na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum Dkt. Dorothy Gwajima.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.