Na. Dennis Gondwe, DODOMA
JUMUIYA ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Dodoma inajivunia kupandisha kiwango cha ufaulu katika mkoa kutoka nafasi ya 23 mwaka jana kwa elimu ya sekondari.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Dodoma, Zuberi White alipokuwa akifungua mkutano wa mwaka wa ALAT mkoa uliofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
White alisema “ALAT Mkoa wa Dodoma tumetekeleza kwa asilimia 90 vikao vyetu vyote vimefanyika kwa mujibu wa ratiba. Kwa upande wa elimu ya sekondari, Mkoa wa Dodoma tumepanda sana. Dodoma tulikuwa nafasi ya 23, ila mwaka tumepanda sana na kukosa pointi moja kuingia 10 bora. Hongera kwa wenyeviti na wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Dodoma kwa kazi nzuri”.
Mwenyekiti huyo aliwashauri wajumbe kuihamasisha jamii ili watoto wasome. “Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutupatia fedha za mapambano dhidi ya UVIKO-19. Mheshimiwa Rais ametusaidia sana katika kukamilisha madarasa. Wanafunzi wote wamepelekwa shule na hatukuwa na chaguo la pili msimu huo” alisema White.
Aidha, aliwakumbusha kuwa uchumi na maendeleo ni mambo yanayokwenda pamoja na kuwasisitiza kuinua uchumi wa wananchi wao. “Karibuni Dodoma Makao Makuu ya nchi. Niwahakikishie ni salama kwa watu wote” alisisitiza White.
Mkutano wa mwaka wa ALAT Mkoa wa Dodoma ulifanyika katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ukitanguliwa na ziara ya siku moja ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa jijini hapo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.