JUMUIYA ya Tawala la Mitaa Tanzania (ALAT) imempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi kwa kuwawezesha wanawake katika Jiji la Dodoma kupitia fursa za mikopo inayotolewa na Halmashauri.
Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Gulam Mukadam alipokuwa akiongea katika uzinduzi wa mradi wa kutokomeza vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto kwenye masoko leo jijini Dodoma na mama Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni rasmi.
Mukadam alisema kuwa changamoto kubwa ni dira ya pamoja katika utokomezaji vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto. Alisema kuwa vitendo hivyo vina athari kwa uchumi wa nchi kwa sababu unyanyasaji na ukatili wa kijinsia unaleta athari ya kimaendeleo kwa wanawake na kuchangia katika uzorotaji wa uchumi wa nchi. Aidha, alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuwa mstari wa mbele katika kuwainua wanawake. “Nimpongeze Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi kwa namna ambavyo amekua msaada kwa akina Mama wa Jiji hili kwa kuwapatia mikopo inayowawezesha kufanya biashara zao. Serikali za mitaa jukumu lao ni kuwawezesha wananchi wao kuzipata fursa” alisema Mukadam.
Mwenyekiti huyo ambaye pia mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga alisema kuwa zipo changamoto ya lugha chafu kwa wanawake katika masoko inapaswa kushughulikiwa na kutokomezwa kabisa. “Tukiwawezesha wanawake na kuwaepusha na vitendo vya unyanyasaji tutakua tunatengeneza Taifa imara na madhubuti na kuweza kufikia azma ya Mheshimiwa Rais ya uchumi wa kati kupitia viwanda," alisema Mukadam.
Mradi wa kutokomeza vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto kwenye masoko unaratibiwa na Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) kwa kushirikiana na wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto na Ofisi ya Rais-TAMISEMI.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.