MWENYEKITI wa Shirikisho la Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) Murshid Ngeze ameimwagia sifa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuwa Halmashauri ya kwanza nchini kujenga na kuwekeza katika miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo hoteli mbili kubwa ambazo ni Dodoma City Hotel yenye ghorofa tisa iliyopo katikati ya Jiji hilo na Government City Complex iliyopo kwenye Mji wa Serikali eneo la Mtumba inayojumuisha hoteli, ukumbi mkubwa wa mikutano unaochukua wastani wa watu 819 kwa wakati mmoja, eneo la mabenki, maduka makubwa, mgahawa, na kumbi zingine sita zenye uwezo wa kuchukua watu 70 hadi 80 kwa wakati mmoja.
Ngeze alitoa sifa hizo mbele ya Baraza la Madiwani la Jiji hilo lililokutana Februari 17, 2022 kupokea na kujadili bajeti ya mwaka ujao wa fedha, ambapo mwenyekiti huyo alikaribishwa ili kuwasalimia wajumbe wa baraza hilo.
Mwenyekiti huyo alisema jiji la Dodoma limeonyesha njia kwa Halmashauri zote nchini na kwamba lengo la Serikali Kuu ni kuona halmashauri zinajitegemea na kujiendesha kwa mapato ya ndani hivyo jiji hilo limewekeza miradi mikubwa katika wakati muafaka.
“Msikate tamaa wala msirudi nyuma, hata pale mnapoyumba kidogo katika makusanyo ya ndani msife moyo kwa sababu mmefanya makubwa sana na shirikisho linaamini mnaweza kufanya vizuri zaidi” alisisitiza mwenyekiti huyo.
Katika mkutano huo, Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma lilipitisha kwa kauli moja bajeti ya Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo zaidi ya shilingi bilioni 100.9 zimeidhinishwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za Halmashauri hiyo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.