HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepongezwa na vijana wajasiriamali wa kikundi cha Youth Entrepreneurship jijini hapo kwa kuwapatia mikopo iliyowawesha kujikwamua kiuchumi na kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana hasa katika kuelekea uchumi wa viwanda kama sera ya awamu ya tano isemavyo.
Shukrani hizo zimetolewa mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), walipotembelea katika mradi unaotekelezwa na kikundi hicho wa kutengeneza majiko ya mkaa unaoendeshwa na vijana hao katika Mtaa wa Nzuguni “B”, Kata ya Nzuguni jijini hapo.
Mwenyekiti wa kikundi hicho, Mariam Mohamed alisema kuwa kikundi kilianzishwa kwa lengo la kuunga mkono jitihada za serikali za kutatua tatizo la ajira kwa wote upande wa wasomi na ambao hawajasoma ili kuwawezesha katika kuwapatia kipato.
“Tunaishukuru Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutuwezesha kupata mtaji, kikundi chetu kilikopeshwa shilingi 4,000,000 awamu ya kwanza mwaka 2018 na tukamaliza marejesho kwa wakati. Pia awamu ya pili tumepata shilingi milioni 20, ambazo zimetusaidia kupata malighafi tunazozihitaji katika kukamilisha shughuli zetu.
“Kikundi chetu kinajishughulisha na utengenezaji wa majiko banifu yanayotumia mkaa kidogo sana, na tulianzisha kikundi tukiwa vijana 7 hivi sasa tumefika 11, wanawake 2 na wanaume 9. Tulianza na mtaji wa shilingi 800,000 na sasa tuna mtaji wa shilingi 30,000,000 ambapo kutokana na faida iliyopatikana kila mwanakikundi amepatiwa shilingi milioni mbili, laki saba, kumi na sita elfu na mia tatu thelathini na tano,” aliongeza Mohamed.
Mbali na mafanikio hayo ya kikundi hicho, mwenyekiti huyo pia alileza changamoto wanazokumbana nazo na kuiomba serikali iweze kuwapatisa usaidizi katika kuzitatua changamoto hizo.
“Tunajitahidi sana katika kuhakikisha tunafanya kazi kwa bidii lakini tunakabiliwa na changamoto kubwa zinazokwamisha maendeleo ya kikundi hiki. Tunakabiliwa na ukosefu wa eneo la kufanyia kazi, barabara mbovu kwani ina mashimo mengi pia miundombinu sio mizuri, mfano daraja likijaa maji gari hazipiti.
“Tunaomba tufikiriwe katika haya kwani kikundi chetu ni moja kati ya kikundi kinachotoa hamasa kwa vijana wengi ili kujiunga katika ufundi wa kutengeneza majiko ili kujipatia kipato binafsi, familia na kuisaidia jamii kiujumla kujikwamua kiuchumi,” alisisitiza Mwenyekiti huyo.
Kikundi cha Youth Entrepreneurship kilianzishwa na vijana wajasiriamali wa kitanzania ambao walinia katika kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za mikono, zinazowasaidia kiuchumi na kuwawezeshe kujiajiri wenyewe na kuwa kikundi cha mfano kwa wajasiriamali wengine kote nchini.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.