Na. Catherine Sungura, WAF-Dodoma
UDHIBITI wa usafi binafsi na usafi wa mazingira unasaidia kupunguza asilimia sabini (70) ya magonjwa ya milipuko yanayotokana na uchafu ikiwemo Kipindupindu.
Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kinga Dkt. Beatrice Mutayoba mara baada ya kufanya usafi kwenye soko la Bonanza lililopo kata ya Chamwino jijini Dodoma ikiwa ni kuelekea wiki ya usafi wa mazingira na matumizi ya choo yanayofanyika kila mwaka kuanzia Novemba 15-19.
“Usafi wa mazingira unasaidia kupunguza asilimia 70 ya magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu hivyo maofisa afya na watendaji wa kata mnapaswa kusimamia vizuri usafi wa mazingira mita tano (5) kuzunguka maeneo ya watu wanayofanyia kazi, ofisini, mashuleni na kwenye nyumba zao ili kuepuka magonjwa ya mlipuko yanayosababishwa na uchafu." Amesema Dkt. Mutayoba.
Aidha, amesema kufanya usafi kwenye mazingira ya kuishi ni jambo jema na kitu kinachosaidia kudhibiti uchafuzi wa vyanzo vya maji chini ya ardhi pamoja na kudhibiti magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu pamoja na magonjwa mengine yanayosababishwa na uchafu.
Dkt. Mutayoba ameongeza kuwa kila eneo lina mwenyewe hivyo ni vyema kusimamia vizuri ili hata usafi wa mwisho wa mwezi au kila jumamosi uweze kusaidia kupunguza kuharibu mazingira.
“Ni vyema sasa kuweka usimamizi kwenye maeneo ya soko ili kuepuka magonjwa ya mlipuko kama kipundupindu pamoja na kusafisha mitaro ya majitaka." Amesema Dkt. Mutayoba.
Hata hivyo Dkt. Mutayoba amewataka maofisa afya pamoja na viongozi wa mitaa na kata kusimamia ujenzi wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa vyoo bora na kuvitumia kwa kuweka miundombinu ya kunawia mikono pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu usafi wa mazingira na usafi binafsi.
Wakati huo huo Dkt. Mutayoba amewataka maofisa afya kusimamia sheria na kanuni za usafi wa mazingira ili kuwadhibiti wale wote wanaojenga kwa kuziba mitaro ya maji kwenye maeneo ya masoko ili kuepuka magonjwa ya milipuko watati wa mvua.
Tukio hili lilihudhuriwa pia na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Prof. Davis Mwamfupe.
Chanzo: wizara_afya (instagram)
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.