Na. Dennis Gondwe, DODOMA
Mamlaka ya Maji safi na Mazingira Dodoma (DUWASA) imepongezwa kwa kujiongeza kutoka vyanzo vyake ya fedha na kufanikisha kufikisha asilimia 95 ya huduma ya maji kwa wananchi wa Ntyuka Chimalaa.
Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Damas Mkassa alipoongoza Kamati ya Siasa Mkoa wa Dodoma kutembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa mfumo wa majisafi Ntyuka Chimalaa.
“Mradi huu usingekuwa umekamilika kama siyo wao DUWASA kujiongeza. Tunamshukuru mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa fedha 359,726,001.49 alizotoa. Lakini kama DUWASA wasingejiongeza tusingefika hapa. Hapa kazi imefanyika yaani kutoka asilimia 0-95, siyo kazi nyepesi. Niwapongeze DUWASA kwa kazi nzuri ya kuchimba visima hapa pamoja na changamoto ya kisima kimoja kutokutoa maji. Hilo ni jambo la kujifunza kwamba ili maendeleo ya wananchi yapatikane ubunifu unatakiwa. Niwaombe wananchi tuulinde huu mradi, tuvilinde vyanzo ambapo vimejengwa visima. Tuepuke uharibifu wa mazingira sababu chanzo kikubwa cha kukosekana kwa maji ni uharibifu wa mazingira. Kutunza visima, maeneo yaliyochimbwa visima, kulinda matenki na kuhakikisha maeneo haya yanakuwa salama na ulinzi shirikishi wa mradi ni kazi yetu” alisema Dkt. Mkassa.
“Katika mradi huu sina jambo la kukosoa nimepanda mwenyewe nimefika juu nimeelezwa mambo ya kitaalam, mifumo ya kutibu maji kabla ya kwenda kuyatumia. Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA yupo vizuri. Nikuombe ubunifu huu uendelee mahali pengine” alisema Mkassa.
Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph alisema kuwa fedha zilipotolewa hazikuweza kutosheleza utekelezaji wa mradi huo. “Tulichofanya DUWASA baada ya kuona tuna mambo mengi na wananchi wanahitaji huduma tukasema lazima yote tuyafanye. Kwa hapa tulipata shilingi milioni 359,726,001.49 kwa ajili ya kutekeleza huu mradi. DUWASA tulitumia mapato yetu ya ndani na vyanzo vingine kuhakikisha tunachimba visima vitatu. Hapa tumeongeza shilingi 112,087,000 kwa ajili ya visima hapa. Maana tungeamua kutumia fedha hizo za UVIKO-19 kwa ajili ya kuchimba visima hata mtandao huu unaoona tumelaza hapa zaidi ya kilometa nne fedha yote ingeishia kwenye kuchimba visima na wananchi wasingeweza kupata maji” alisema Mhandisi Joseph.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kutoa fedha kwa ajili ya kutatua changamoto ya maji. “Mama zetu wanatumia muda mwingi kutafuta maji ili afya ya familia iwepo. Huu ni ukombozi mkubwa sana kwa wananchi wetu. Bado tunamahitaji mengi ya maji, tunafahamu program za maji za serikali za kutoa maji Ziwa Victoria, pale Falkwa na kutoa maji bwawa la Mtera yote ni dhamira njema ya serikali ya awamu ya sita ya Samia Suluhu Hassan kuhakikisha wananchi wanapata maji tena salama na yakutosha yaweze kupatikana makao makuu ya nchi. Tunayahitaji kwenye hospitali, ujenzi unaoendelea na katika kutunza mazingira na bustani” alisema Shekimweri.
Mnufaika wa mradi huo, Zena Bakari alisema kuwa mradi wa maji utawasaidia kuepuka kufuata maji umbali mrefu. Alisema kuwa maji hayo kusogezwa jirani na makazi yao kutawawezesha kutumia muda wao kufanya shughuli za maendeleo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.