ASKOFU wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT), Dkt. Dickson Chilongani (pichani) amefupisha semina ya Maaskofu na Wachungaji 400 ili washuhudie mbashara tukio la kihistoria la kuapishwa kwa Rais John Pombe Joseph Magufuli linalofanyika kwa mara ya kwanza nje ya Dar es Salaam katika mkoa wa Dodoma.
Akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa, Dkt. Binilith Mahenge jijini hapa, Askofu Dkt. Chilongani amesema, asingependa maaskofu na wachungaji waikose fursa hiyo adhimu ya kihistoria ya kushuhudia kuapishwa kwa kiongozi wa nchi katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma, tukio ambalo linafanyika kwa mara ya kwanza mkoani hapa tangu Tanzania kupata Uhuru, Desemba 9, 1961.
Askofu Dkt. Chilongani amesema badala semina hiyo kufanyika kwa siku tatu, watafanya kwa siku mbili hadi Jumatano, ili Alhamisi Novemba 5, mwaka huu, wahudhurie tukio hilo la kihistoria la kuapishwa kwa Rais wa awamu ya tano kushika madaraka kwa kipindi cha pili.
Askofu huyo amesema alimemua kufupisha semina hiyo inayohusu utawala bora ili maaskofu na wachungaji 400 kutoka Dodoma Mjini, Chamwino na Bahi ili wakapate kuona mbashara namna kiongozi aliyeshinda kwa kishindo kwa asilimia 84.4 katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu anavyoapishwa katika viwanja vya Jamhuri, jijini Dodoma.
Askofu Dkt. Chilongani amempongeza Mkuu wa Mkoa, Dkt. Mahenge kutokana na kusimamia amani na utulivu wakati wa uchaguzi ambapo Rais Magufuli alipata ushindi wa kishindo na inawezekana mkoa wa Dodoma umeongoza kwa kumpa kura nyingi.
Alisema hiyo ni fursa ya kihistoria kwa maaskofu na wachungaji hao kuhudhuria kuapishwa kwake ili wakamsikilize kiongozi huyo bora na kusikiliza malengo yake ya baadaye katika uongozi wake.
Askofu Dkt. Chilongani amesema Rais Magufuli ameshinda kwa kishindo kutokana wananchi kuwa na imani naye lakini pia alifanya kampeni za kistaarabu, si kwa matusi wala kunyanyasa, alikuwa akielezea mambo aliyofanya na malengo yake ya baadaye.
“Keshokutwa wakati Rais Magufuli anaapishwa, maadamu tupo kilometa chache kutoka hapa, sisi maaskofu na wachungaji ni vizuri tuende tukashuhudie na kumsikiliza atasema nini na tukasikilize mipango yake ya baadaye,” amesisitiza kiongozi huyo.
Akizungumza wakati wa kufungua warsha hiyo, Mkuu wa Mkoa, Dkt. Mahenge alilipongeza Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika kutokana na mchango wake mkubwa katika masuala ya afya na elimu.
Amemshukuru Askofu kwa pongezi hizo kwa ushindi wa Magufuli ambao unaonesha imani ya Watanzania kwa kiongozi huyo kutokana na kazi nyingi za maendeleo alizozifanya.
Pia alimpongeza Askofu huyo kwa kupunguza siku ya warsha ya utawala bora ili kuwapa nafasi maaskofu 400 kuhudhuria kuapishwa huko akasema atashirikiana na Mkuu wa Wilaya, Josephat Maganga kuhakikisha wanapata nafasi ya kuingia uwanjani.
Aidha, amewapongeza kwa mchango wao katika sekta ya afya, kwa kujenga hospitali ya Mvumi, kituo cha Mackay na Hombolo pamoja na vituo vya magonjwa ya macho.
Aliwapongeza viongozi wa kanisa kwa kazi nzuri waliyofanya wakati wa kampeni kwani wakati wote walikuwa wakifanya maombi na wakashiriki katika kuombea uchaguzi huo ukafanyika, kwa maombi yao wametoa mchango mkubwa kushirikiana na serikali.
Akifafanua zaidi amesema kanisa hilo limetoa mchango mkubwa katika elimu kuanzia ya msingi na vyuo vikiwamo vya afya na pia wanaendelea kuanzisha kozi mpya kwa ajili ya kusaidia jamii kupata elimu.
Dkt. Mahenge amesema katika suala la utawala bora linahusisha demokrasia, utawala wa sheria, haki na usawa, ushirikishaji wananchi, uwajibika na uwazi na kwa ujumla wake penye utawala bora ndiyo panapopatikana maendeleo.
"Serikali ya awamu ya Tano, ya Rais John Magufuli imejitahidi kutekeleza utawala bora ukiwemo wa kurejesha nidhamu ya kazi, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, utunzaji wa raslimali za umma ambazo zimesaidia katika kuongeza huduma kwa umma kwa kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo reli, barabara, madaraja na miundombinu mingine.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini, Josephat Maganga aliwapongeza viongozi kwa kazi nzuri wanazofanya, akawakata waendelee na utaratibu wa kushirikiana na serikali katika kufanya kazi zake mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge akiongea mbele ya Maaskofu na wachungaji wapatao 400 wanaohudhuria semina kuhusu utawala bora.
Maaskofu na Wachungaji kutoka Dayosisi ya Central Tanganyika wanaohudhuria semina ya utawala bora (Pichani juu na chini).
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.