TIMU ya soka inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dodoma Jiji FC imeibana mbavu timu ya Azam FC na kugawana alama moja katika mchezo uliochezwa ndani ya dimba la Jamhuri mchezo uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2 katika mchezo uliokuwa na ufundi aina yake.
Azam ndiyo walikuwa wa kwanza kupata goli katika dakika ya pili ya mchezo kupitia kwa mchezaji wao Prince Dube, goli ambalo lilidumu mpaka muda wa mapumziko, ambapo katika kipindi cha pili dakika ya 70 Dodoma Jiji walipata goli la kusawazisha kupitia kwa Seif Karihe aliyeingia akitokea benchi na mnamo dakika ya 77 ya mchezo Anuary Jabir alipachika goli la pili kwa walima zabibu na kuwafanya kuongoza mpaka dakika 90 za mchezo na kuongezwa dakika 5 zilizowapa nafasi Azam kupata goli la kusawazisha kupitia kwa Obrey Chirwa.
Akizungumza baada ya mchezo huo Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji FC Mbwana Makata alisema kuwa vijana wake wamepambana lakini ukosefu wa umakini katika dakika za mwisho ndiyo umepelekea wao kukosa pointi tatu na kuambulia moja wakiwa nyumbani.
Dodoma Jiji ambao walionesha kabumbu safi mwanzo hadi mwisho wa mchezo sasa wamefikisha alama 38 wakiwa katika nafasi ya 6 ya msimamo wa ligi huku wakicheza michezo 27 na tayari wameanza maandalizi ya mchezo dhidi ya Simba SC siku ya Jumanne Aprili 27, 2021 kwenye dimba la kumbukumbu ya Benjamin Mkapa Mkoani Dar es salaam.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.