Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WENYEVITI na wakurugenzi wa halmashauri nchini wametakiwa kuichambua bajeti iliyopitishwa na serikali ili wananchi katika ngazi za chini wawe na uelewa na kunufaika nayo.
Agizo hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), Murshid Ngeze alipokuwa akiongea katika Mkutano wa mwaka wa ALAT tawi la Mkoa wa Dodoma uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma mwishoni mwa wiki.
Ngeze alisema kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imepitisha bajeti ya kihistoria na ya mfano. “Ndugu zangu, bajeti hiyo imejaa fursa mbalimbali zenye manufaa kwa halmashauri zetu na wananchi wetu. Wenyeviti wote na wakurugenzi wa halmashauri ni wajibu wenu kuichambua bajeti hiyo na kuwaeleza wananchi ili fedha zitakapokuja kwenye halmashauri zetu ziweze kuwanufaisha na sisi kuzisimamia ipasavyo” alisema Ngeze.
Aidha, aliwataarifu wajumbe kuwa Mkoa wa Kagera umepata shilingi bilioni 70 kwa ajili ya kuanzisha ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba. Alishauri kuwa Mkoa wa Dodoma kujipanga kwa ufugaji huo kutokana na kutokuwa na bahari wala ziwa. Ufugaji huo ni wa kawaida na hauhitaji uwekezaji mkubwa, aliongeza.
Awali akimkaribisha Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Dodoma, Zuberi White alisema kuwa ALAT Mkoa wa Dodoma ni wamoja na wanafanya kazi kwa ushirikiano.
Mkutano wa mwaka wa ALAT Mkoa wa Dodoma ulifanyika katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ukitanguliwa na ziara ya siku moja ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa jijini hapo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.