Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MPANGO na Bajeti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma imejikita katika kuimarisha elimu ya awali na msingi kwa lengo la kuwahakikishia wanafunzi elimu bora na mazingira mazuri.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alipokuwa akielezea vipaumbele vya Mpango na Bajeti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa waandishi wa habari.
Mafuru alisema kuwa kipaumbele kwenye Mpango na Bajeti ya Halmashauri ya Jiji kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ni kuimarisha elimu ya awali na msingi. “Leo hii ukienda kwenye maeneo mengi bado tunachangamoto katika elimu ya awali na msingi. Elimu bure imetusaidia sana. Watoto wengi wamepata fursa ya kuja shuleni. Tumeandikisha watoto wengi zaidi ya asilimia 87 wa shule ya awali na asilimia 93 shule ya msingi. Ongezeko hili linasababisha kuwa na upungufu wa madarasa na madawati” alisema Mafuru.
Alisema kuwa katika kipindi cha miezi sita iliyobaki kukamilisha mwaka wa fedha 2022/2023 halmashauri yake inaendelea kujenga madarasa harakaharaka na madawati. “Na kuanzia mwezi Julai mwaka wa fedha 2023/2024 kasi kubwa ya fedha tutaipeleka kwenye maeneo hayo. Bajeti hii inakwenda kuwahakikishia mazingira bora ya kujifunzia wanafunzi” alisisitiza Mafuru.
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma lilipitisha makisio ya Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/2024 jumla ya shilingi 128,278,555,369. Kati ya fedha hizo, shilingi 55,128,229,369 ni mapato ya ndani na shilingi 59,082,835,000 ni ruzuku ya mishahara. Ruzuku ya matumizi mengineyo ni shilingi 1,005,792,000 na shilingi 13,061,699,000 ni ruzuku ya miradi ya maendeleo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.