BAJETI ya Shilingi Bilioni 180 ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma iliyopitishwa na Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo jana kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za Halmashauri kwa Mwaka ujao wa Fedha imesisimua wajumbe wa Baraza hilo na Wananchi wengine kwani imelenga kumaliza kabisa baadhi ya changamoto ikiwemo zilizopo kwenye Sekta ya Elimu ambayo pekee imetengewa zaidi ya Shilingi Bilioni nane.
Katika Mkutano wa Baraza hilo uliofanyika jana katika ukumbi wa Jiji hilo, Baraza limepitisha bajeti hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 ambapo Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Godwin Kunambi aliwasilisha Bajeti nzima mbele wajumbe wa Baraza hilo lenye Madiwani 60.
Kunambi alisema bajeti ya Makusanyo yanayotokana na vyanzo vya ndani vya Halmashauri hiyo yanatarajiwa kuwa Shilingi Bilioni 72, ikiwa imeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 68 za Mwaka huu unaondelea.
“Mheshimiwa Mwenyekiti na wajumbe, tukiangalia makusanyo yetu ya ndani kwa bajeti ya Mwaka tulionao sasa ni Bilioni 68, lakini kwa Mwaka ujao tanatarajia kukusanya takribani Bilioni 72 hivyo kuna ongeza la Shilingi Bilioni tano” alisema Kunambi.
Alisema moja ya vipaumbele katika Mpango wa Bajeti hiyo ni kuboresha Sekta ya Elimu ambapo jumla ya Shilingi Bilioni nane zimetengwa.
Mkurugenzi Kunambi alisema Halmashauri anayoiongoza inakusudia kujitegemea na kujiendesha yenyewe kwa asilimia 100 kuanzia Mwaka 2021/2022 ambapo itaachana kabisa na kutegemea ruzuku kutoka Serikali Kuu.
“Tunaposema Halmashauri kujitegemea na kujiendesha yenyewe maana yake ni kwamba tutatekeleza miradi ya Maendeleo katika Kata zetu kwa Fedha za ndani, tutalipa Mishahara ya watumishi wetu wote kwa Fedha za ndani, pamoja na kulipa stahiki mbalimbali za Watumishi…tunakusudia kufikia hatua hii” alifafanua.
Wakichangia hoja hiyo, baadhi ya wajumbe wa Baraza la Halmashauri hiyo wakiongozwa na Mstahiki Meya Profesa Davis Mwamfupe walielezea kufurahishwa kwao na vipaumbele na ukubwa Mpango na Bajeti hiyo kwani wanaamini utaharakisha maendeleo kwa Wananchi wanaoowaongoza.
Mbunge wa Jimbo la Dodoma ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Vijana Ajira na Watu Wenye Ulemavu Anthony Mavunde alisema Bajeti iliyopitishwa inagusa maisha na itaboresha Sekta muhimu ikiwemo Elimu, Afya, na Maji.
“Bajeti hii kwenye Elimu pekeake imetengwa zaidi ya Bilioni nane na hata ukiangalia kwenye Sekta ya Afya kiasi kilichotengwa ni Bilioni Mbili ambacho ni kiasi kikubwa sana …hii itasaidia kujibu kwa vitendo hoja za matumizi ya makusanyo makubwa tunayoyakusanya…hii ni bajeti ambaye kila anayeipenda Dodoma atakubali kuwa ni nzuri” alisema Mavunde.
Mavunde alisema Halmashauri ya Jiji la Dodoma ndiyo ya kwanza nchini kutenga kiasi kikubwa cha Fedha kwa ajili ya kuwezesha Makundi Maalum ikiwemo watu wenye ulemavu ambao katika Bajeti hiyo wametengewa Shilingi Bilioni 3.3 ambazo zikitolewa kwa walengwa Halmashauri itakuwa imefanya jambo kubwa la kupigiwa mfano.
“Mheshimiwa Mwenyekiti mimi hili ni eneo langu la kazi kule Serikalini na nafahamu changamoto ni kubwa kwenye uwezeshaji, tukienda katika kumbukumbu sisi tutakuwa Halmashauri ya kwanza nchi nzima ambaye tumetenga Fedha nyingi katika makundi haya maalum” alisema Mavunde.
Kwa upande wake Mstahiki Meya Prof. Mwamfupe (Pichani juu) alisema bajeti ya hiyo ni yenye kuacha alama kwani haijawahi kutokea siku za nyuman na kwamba wamefikia hatua hiyo kutokana na juhudi na uzalendo wa Wanadodoma wote.
Alisema Jiji la Dodoma linatakiwa kuwa la mfano ili kuunga mkono juhudi kubwa za Seriikali katika utoaji wa huduma za Kijamii na kwamba ushirikiano na uzalendo kwa wadau ndiyo silaha pekee.
Naye Anselem Kutika ambaye ni Dwani wa Kata ya Kikuyu Kusini alisema anaunga mkono bajeti hiyo kwani haijawahi kutokea huku akitoa pongezi kwa wataalam wote wa Jiji wakiongozwa na Mkurugenzi Kunambi.
“Mheshimiwa Mwenyekiti kabla ya yote nianze kwa kusema kuwa, kwa niaba ya Wananchi ya Kikuyu Kusini naunga mkono bajeti hii kwa asilimia 100…hii ni bajeti ya Wananchi kwani imegusa maisha yao” alisema Kutika wakati akichangia hoja hiyo ya Bajeti.
Bajeti iliyopitishwa na Baraza hilo jana inatarajiwa kuendelea kujadiliwa katika ngazi mbalimbali za juu kabla ya kuanza kutumika mapema Mwezi Julai Mwaka huu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.