BAJETI ya matengenezo na ukarabati wa barabara na madaraja kwa mkoa wa Dodoma imeongezeka kutoka Shilingi bilioni 12.7 mwaka 2020/2021 hadi kufikia Shilingi bilioni 66. 2 mwaka 2023/24.
Hayo yameelezwa na Meneja wa TARURA mkoa wa Dodoma, Mhandisi Edward Lemelo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya ofisi yake katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita.
Mhandisi Lemelo amesema ongezeko hilo la bajeti kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi 2023/2024 ambalo limeongezeka kwa asilimia 412.77 tangu Rais Samia alipoingia madarakani 2021 limesaidia kuimarika kwa ubora wa mtandao wa barabara za lami kutoka Km 171.29 hadi Km. 309.71.
“Barabara za changarawe zimeongezeka kutoka Km 1,258.65 hadi Km 1,827.5 madaraja 19, maboksi kalavati 45 na mitaro yenye urefu wa mita 73,822.24 imejengwa, taa za barabarani 470 zimesimikwa, barabara mpya zenye urefu wa Km 544.60 zimefunguliwa ambazo hazikuwepo kabisa”, alisema.
Amesema kuwa mtandao wa barabara zenye hali nzuri zimeongezeka kutoka asilimia 10, Februari 2021 hadi kufikia asilimia 34.70 Machi 2024. Vilevile katika kipindi hicho cha miaka mitatu ya serikali ya awamu ya sita TARURA mkoa wa Dodoma imeongeza vitendea kazi pamoja na kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi.
“Magari nane mapya yamenunuliwa na kusambazwa katika ofisi za Mameneja wa wilaya na mkoa, ununuzi wa mitambo ya ujenzi wa barabara ikiwemo ‘Motor Grader’, ‘Roller’, ‘Bulldozer’ na ‘Excuvator’ na ‘Loadbed’ vimenunuliwa na kukabidhiwa kwa Meneja wa wilaya ya Chamwino ununuzi wa vitendea kazi ambavyo vimerahisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi wa kazi za Wakala” alisisitiza.
Mhandisi Lemelo ameongeza kuwa Wakala umetekeleza miradi ya kielelezo ikiwemo ujenzi wa barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba Km 12.6, ujenzi wa barabara ya lami Mwanga-Kisasa-Medeli Km 10.7, ujenzi wa barabara ya lami Swaswa-Mpamaa-Arusha Road Jct Km 8.2, ujenzi wa barabara ya lami ya mzunguko Mlimwa Km 1.55, ujenzi wa barabara katika Soko la Machinga Km 0.6 na ujenzi wa barabara ya kuzunguka makazi ya Waziri Mkuu Km 2.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.