Asilimia 72 ujenzi wa Barabara ya Mwangaza-Kisasa Medeli
Imewekwa tarehe: February 13th, 2023
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MRADI wa ujenzi wa Barabara ya Mwangaza-Kisasa Medeli Kilometa 10.7 kwa kiwango cha lami umetekelezwa kwa asilimia 72 ukitarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2023.
Kauli hiyo ilitolewa na Mhandisi wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini Wilaya ya Dodoma (TARURA), Kasongo Mojiro alipokuwa akisoma taarifa ya ujenzi wa Barabara ya Mwangaza-Kisasa Medeli kilometa 10.7 kwa kiwango cha lami kwa Kamati ya Siasa ya Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma iliyotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo.
Mhandisi Mojiro alisema kuwa barabara hiyo inajengwa kwa shilingi 10,397,184,981 fedha kutoka serikali kuu. Alisema kuwa mradi ni wa miezi 18 na ulianza kutekelezwa tarehe 24 Januari, 2022 na utakamilika tarehe 23 Julai, 2023. “Kazi zilizotekelezwa ni uwekaji wa lami kilometa 6.7, uwekaji wa tabaka la changarawe kilometa 7.4. Ujenzi wa makalavati na madaraja umekamilika. Kazi ya kusafisha km 3.3 unaendelea” alisema Mhandisi Mojiro.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dodoma, Charles Mamba alisema kuwa kazi iliyofanyika ni nzuri na barabara inajengwa kwa kiwango kizuri. Alisema kuwa lengo la serikali ni kuboresha miundombinu ya usafiri ili kuwawezesha wananchi kusafiri na kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi.