RAIS Dkt. John Pombe Magufuli amepongezwa kwa ujenzi wa miundombinu nchini na kurahisisha huduma ya usafiri nchini wakti Mwenge wa Uhuru ukiendelea kupitia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Wilaya ya Dodoma Mjini.
Pongezi hizo zilitolewa na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Mzee Mkongea Ali baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa Barabara ya Kikuyu-Chidachi-Kinyambwa-Itega kwa kiwango cha lami na kuweka jiwe la msingi mradi huo katika mbio za Mwenge wa Uhuru unaokimbizwa Wilaya ya Dodoma mjini leo.
Ali alisema “napenda nimpongeze Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya katika nchi hii. Mheshimiwa anafanyakazi kubwa katika ujenzi wa miundombinu ili kuboresha maisha ya wananchi na kurahisisha usafiri wao”. Katika uongozi wake, nidhamu kwa watumishi wa umma imerudi na wanafanya kazi kwa weledi" aliongeza.
Awali akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa barabara ya Kikuyu-Chidachi-Kinyambwa-Itega kwa kiwango cha lami, Mhandisi Emmanuel Manyanga alisema kuwa ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa km 6 unatekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Lengo kuu la mradi huu ni kuboresha miundombinu ya jiji pamoja na kuwezesha mawasiliano baina ya wakazi wake kutoka eneo moja kwenda eneo lingine pamoja na kufika katikati ya Jiji la Dodoma ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii” alisema Mhandisi Manyanga.
Akiongelea utekelezaji wa mradi huo, alisema kuwa kazi ya ujenzi wa barabara hiyo inafanywa na Mkandarasi M/S STECOL Corporation kutoka China kwa gharama ya Shilingi 9,413,277,014.17.
Alisema kuwa kazi za ujenzi wa barabara zilianza tarehe 01/07/2018 kwa mkataba wa miezi kumi na tano (15) hivyo, kazi hiyo inatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30/09/2019. “Hivi sasa Mkandarasi yupo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa kazi za ujenzi wa barabara hii ambao umefikia asilimia 80 na kazi zilizobakia ni ukamilishaji wa mitaro ya maji ya mvua pamoja na njia za watembea kwa miguu, uwekaji wa taa za barabarani zenye kutumia mfumo wa umeme jua, vibao vya alama za barabarani na uchoraji wa alama za mistari ya barabara. Mkandarasi hadi hivi sasa amekwisha lipwa kiasi cha Shilingi 5,550,088,642.96” alisema Mhandisi Manyanga.
Kuhusu changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa mradi huo, alizitaja kuwa ni uwepo wa miundombinu ya maji ardhini ambayo ilikuwa ni vigumu kuitambua kutokana na kutokuwa na alama na kumbukumbu ya kutambulisha uwepo wa miundombinu hiyo. Aliongeza kuwa changamoto hiyo ilipelekea baadhi ya mabomba ya maji safi kukatwa mara kwa mara wakati wa uchimbaji kwa kutumia mitambo na kupelekea adha kwa wakazi na watumiaji wa huduma hiyo ya maji.
Katika salamu za Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini, Anthony Mavunde, alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma itaongoza kwa kuwa na mtandao mrefu zaidi wa barabara za lami nchini kwa Halmashauri. “Halmashauri ya Jiji la Dodoma tutaongoza kwa kuwa na mtandao mrefu wa barabara za lami Tanzania. Halmashauri ya Kinondoni ina kilimeta 136, wakati Halmashauri ya Jiji la Dodoma ina urefu wa kilimeta 130.5 hivyo, kilometa 26 zinazojengwa zikikamilika Halmashauri ya Jiji tunakwenda kuweka historia ya kuwa na mtandao mrefu zaidi wa barabara za lami kwa Halmashauri” alisema Mavunde.
Ikumbukwe kuwa mradi huo umefadhiliwa na Serikali kuu ya Tanzania kupitia mkopo wa benki ya Dunia.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge 2019 ndugu Mzee Mkongea Ali alifurahia kwa kupiga makofi baada ya kuzindua barabara ya lami Chidachi.
Gari maalum zenye wakimbiza Mwenge zikiondoka kwenda kufanya ukaguzi wa barabara.
Wakimbiza Mwenge wa Uhuru 2019 wakiendelea na ukaguzi wa miundombinu ya barabara, hapa wakikagua 'kalavati'.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.