Na. Abdul Juma, MIYUJI
Diwani wa Kata ya Miyuji, Beatrice Ngerangera amesema ujenzi wa Barabara ya kilometa sita ya kutoka Miyuji hadi Ipagala umesaidia kufikisha huduma za kijamii kwa wananchi na kuharakisha usafiri katika mazingira bora na salama.
Kauli hiyo aliiotoa alipokuwa akiwaelezea waandishi wa habari mafanikio ya serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha miaka minne katika Kata ya Miyuji.
Ngerangera alisema kuwa kilio kikubwa cha wananchi wa Miyuji ilikuwa ni barabara. “Nitumie fursa hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika utawala wake, Kata ya Miyuji imepata mambo mengi mazuri hasa ujenzi wa Barabara. Hapo zamani ilikuwa ni vigumu kupita kwenye barabara hii ila hivi sasa tunapita kwa amani. Mradi wa barabara hii yenye urefu wa kilomita sita, inaunaganisha kati ya Kata ya Miyuji na Ipagala. Hivyo, umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 6.7. Awali wananchi walikuwa wakipata taabu wakati wa mvua. Mimi, najisikia vizuri, kipekee nimpongeze mama, rais wa wanyonge kwakuwa amesikia kilio chetu niseme Mungu ambariki sana”.
Akiongelea faida za barabara hiyo alizitaja kuwa ni kuondoa changamoto ya kina mama kujifungulia njiani. “Hakuna kuharibika kwa vyombo vya usafiri, pia ajali zimepungia, zamani watu walikuwa wanafia njiani kwasababu ya ubovu na ufinyu wa barabara wakiwa wanafuata huduma ya afya katika hospitali ya St. Gemma” alisema.
Nae Mwenyekiti wa Mtaa wa Miyuji Proper, Hawardi Mbogela aliipongeza serikali ya awamu ya sita na Mbunge, Anthony Mavunde kwa kuweza kutimiza ahadi ya kuwajengea barabara yenye kiwango cha lami. “Rais wetu amekuwa akisikiliza sana kilio cha wananchi wake, sisi kama viongozi wa kata hii tulikaa pamoja na diwani tukawasilisha suala hili kwenye uongozi wa juu, hatimae limetekelezwa kwa asilimia miamoja. Hivyo, nimpongeze Rais mama Samia na mbunge wetu Mavunde bila kusahau Diwani wa Miyuji, Beatrice” alisema Mbogela.
Kwa namana nyingine wakazi wa Kata ya Miyuji waliweza kueleza ni kwa namna gani wamefurahi kwa kutekelezwa kwa mradi huo wa ujenzi wa barabara katika kata yao kwasababu mradi huo umekuwa fursa katika kata yao.
Akizungumza mkazi wa Miyuji Proper, Maria Juma aliishukuru serikali kwa kusikiliza malalamiko yao kwa kuwajengea barabara iliyowaunganisha na Kata ya Ipagala. “Kwa kweli tunamshukuru Mungu kwaajili ya barabara hii. Pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa sababu barabara hii imetunufaisha sisi wananchi wa Miyuji. Kabla ya barabara hii hali ilikuwa mbaya hapa katika kata yetu kulikuwa na makorongo hata wananchi wengine walifia njiani na kujifungulia wakiwa wanaenda katika Hospital ya St. Gemma kupata huduma,” alisema Juma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.