Na. Prisca Maduhu, TAMBUKARELI
MRADI wa Barabara ya Mwangaza-Kisasa Medeli Kilometa 10.7 kwa kiwango cha lami ni muhimu kwa sababu inagusa kata tatu, ikitoa afueni kwa Barabara kuu ya Dodoma -Morogoro kwa kuwaondolea foleni wananchi wa Wilaya ya Dodoma na kuwaletea maendeleo.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alipokuwa akimkaribisha Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, kukagua barabara hiyo.
Alhaj Shekimweri alisema kuwa barabara hiyo inahudumia kata tatu na kupunguza foleni kwa Barabara ya Dodoma -Morogoro na barabara inayoelekea Chuo Kikuu cha Dodoma ikitokea Jakaya Kikwete Convention Center. “Barabara hii inaongeza thamani ya nyumba 300, inaongeza thamani ya eneo la Mwangaza na eneo la Medeli. Pia ni njia ya mchepuko kuwahi kufika Hospitali ya Benjamini Mkapa na Chuo Kikuu cha Dodoma. Barabara inaongeza thamani kwa eneo la Njedengwa Investment Area lililotengwa kwa ajili ya hoteli za kitalii na taasisi mbalimbali zimeshajenga kama Mfuko wa Barabara na Tume ya Taifa ya Uchaguzi” alisisitiza Alhaj Shekimweri.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Tambukareli, Juma Michael alimshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa barabara hiyo. “Tunamshukuru Rais wa serikali ya awamu ya sita, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea mradi huu mkubwa sana wa barabara kutokana na fedha za tozo ya mafuta. Kwa niaba ya wananchi wa Kata ya Tambukareli tunamshukuru sana. Barabara hii itaongeza kasi ya ukuaji wa maendeleo kwa kuwapunguzia wananchi muda wa kukaa kwenye foleni barabarani” alisema Michael.
Akisoma taarifa ya mradi huo, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), Wilaya ya Dodoma, Mhandisi Kasongo Morijo alisema kuwa ujenzi wa Barabara ya Mwangaza-Kisasa Medeli Kilometa 10.7 kwa kiwango cha lami unagharamiwa na serikali kupitia fedha za tozo ya mafuta. “Gharama za mradi ni shilingi 10,397,184,981 chini ya Mkandarasi China Henan International Cooperation Group Co. Ltd (CHICO) kwa muda wa miezi 12” alisema Mhandisi Morijo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.