UJENZI wa barabara za kiwango cha lami katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma wenye gharama ya bilioni 88.1 zikiwa na urefu wa kilomita 51.2 umefikia asilimia 56 na unatarajiwa kukamilika mwezi Julai mwaka huu huku zikiunganisha Wizara zote ndani ya Mji huo.
Hayo yamesemwa na Katibu wa kuratibu mchakato wa Serikali kuhamia Dodoma na Uratibu wa ujenzi wa mji wa Serikali, Meshack Bandawe wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hizo jijini Dodoma.
“Sasa hivi kinachoendelea ni ujenzi wa barabara za lami zinazozunguka ndani ya mji wa Serikali na ujenzi huu umefikia sehemu nzuri na ikifika Julai mwaka huu utakuwa umekamilika” alisema Bandawe.
Aidha, mratibu huyo alisema ujenzi huo unahusisha ujenzi wa barabara za njia mbili za urefu wa kilomita 22.4 na zile zenye njia moja zenye urefu wa kilomita 28.8, pamoja na ujenzi wa miundombinu mingine kama maji, umeme, gesi, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), zimamoto na uokoaji, maduka makubwa, pamoja na huduma za treni.
Katika hatua nyingine, Bandawe alisema ujenzi wa ofisi awamu ya pili utaanza baada ya kupata kibali hivi karibuni.
Mradi wa ujenzi wa barabara za Mji wa Serikali Mtumba unatekelezwa na mkandarasi China Heinan International Cooperation Co. Ltd (CHICO) na unasimamiwa na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), ulizinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli mwezi Machi 2019.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.