Serikali imeuagiza uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuhakikisha Baraza la Biashara la Wilaya linakutana na kutatua changamoto za wafanyabiashara kwa mujibu wa taratibu.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama alipotembelea kituo cha kutoa mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana (JOWOG) kilichopo Kata ya Hombolo Jijini hapa.
Waziri Mhagama alisema kuwa mabaraza ya biashara yanamchango mkubwa katika kutatua changamoto za wafanyabiashara. “Niendelee kuwaomba Halmashauri na viongozi wote mliohapa, tunatakiwa kuendelea kuzingatia uendeshaji wa mabaraza yetu ya biashara. Mabaraza ya biashara ya Mkoa ni lazima yaketi na mabaraza ya biashara ya Wilaya ni lazima yaketi” alisema Waziri Mhagama.
Waziri huyo aliyataka mabaraza hayo kuhakikisha maazimio yanafikishwa ngazi za chini za utekelezaji. “Jambo la msingi siyo kuhakikisha mabaraza yanakutana tu, kukutana ni jambo jingine lakini utekelezaji wa maazimio yanayotokana na mabaraza hayo. Maazimio waheshimiwa madiwani msimamie yashuke mpaka ngazi ya chini ya utekelezaji. Nimesema uendeshaji huo wa mabaraza upo kwa mujibu wa Waraka namba 1 wa Mwaka 2001, Waraka wa Rais na tayari Waraka huo ulishatangazwa kwenye gazeti la serikali namba 39, kwa hiyo tayari ni sheria, ni lazima mhakikishe mikoa na wilaya zinaendesha mabaraza hayo” alisisitiza Waziri Mhagama.
Waziri Mhagama alishauri ziendelee kutumika fursa zilizopo kutatua changamoto katika eneo la uwekezaji nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama akipata maelezo kutoka kwa mtumishi wa kituo cha kutoa mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana (JOWOG) kilichopo Kata ya Hombolo Jijini hapa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.